Mashambulizi ya anga yapiga miji ya Sanaa na Hodeidah ya Yemen wakati uhasama ukizidi kupamba moto (6)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 27, 2026
Mashambulizi ya anga yapiga miji ya Sanaa na Hodeidah ya Yemen wakati uhasama ukizidi kupamba moto
Picha hii ikionesha athari za baada ya mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia yaliyolenga kiwanda na maghala yanayotumika kusindika viazi jijini Sanaa, Yemen, Novemba 26, 2026. (Picha na Mohammed Mohammed/Xinhua)

SANAA - Wimbi jipya la mashambulizi ya anga limeipiga Sanaa, mji mkuu wa Yemen, na mji wa bandari wa Hodeidah kwenye Bahari ya Shamu jana Alhamisi, likiwaacha watu wasiopungua watano wakiwa wamejeruhiwa, wakiwemo wazima moto wawili, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kundi la Wahouthi na vyanzo vya habari nchini humo.

Kituo cha televisheni cha al-Masirah kinachoendeshwa na kundi la Wahouthi kimeilaumu Saudi Arabia kwa mashambulizi hayo, kikisema wafanyakazi wanawake watatu wamejeruhiwa wakati mashambulizi matatu ya anga yalipopiga kiwanda cha kusindika viazi na maghala yake karibu na Mzunguko wa Barabara wa Amran katika wilaya ya Bani al-Harith, kaskazini mwa Sanaa.

Mamlaka ya Ulinzi wa Raia inayoendeshwa na kundi la Wahouthi imesema Alhamisi kuwa timu zake zililengwa na mashambulizi mengine ya anga "wakati zikizima moto" katika wilaya hiyo, yakijeruhi wazima moto wawili na kuharibu magari ya zima moto.

Halikadhalika, wakazi wa Hodeidah pia waliripoti milipuko mikubwa siku hiyo ya Alhamisi. "Milipuko mitatu mfululizo imetikisa nyumba yangu nzima," mkazi mmoja wa mji huo wa pwani ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Mashuhuda katika mji huo wa Hodeidah walisema siku hiyo ya Alhamisi kuwa mashambulizi ya anga yalilenga jengo la chuo cha jeshi la majini kwenye pwani ya mji huo, huku kukiwa na taarifa za awali kuhusu majeruhi na vifo.

Wakati huo huo, katika taarifa iliyopokelewa na Xinhua, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema siku hiyo ya Alhamisi kuwa, ikifanya kazi ya mpatanishi asiyeegemea upande wowote, imewezesha uhamishaji wa mabaki ya miili ya binadamu kuvuka mistari ya mbele ya mapigano nchini Yemen kuanzia Jumanne hadi Alhamisi kwa ombi la pande zinazohusika katika mgogoro huo.

ICRC imesema operesheni hiyo inafuatia ahadi zilizotolewa na pande husika katika mgogoro huo Desemba 2025, wakati ziliposaini tamko la pamoja la kanuni juu ya usimamizi kwa heshima wa miili ya marehemu na mabaki ya binadamu huko Muscat, mji mkuu wa Oman.

Mwenendo huo wa sasa wa hali unajiri huku uhasama ukizidi kupamba moto kati ya kundi hilo la Wahouthi la Yemen na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Katika siku za hivi karibuni, Wahouthi wamedai kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kwa makombora na droni dhidi ya viwanja vya ndege, bandari, na miundombinu ya nishati ya Saudi Arabia; wakati huo huo, vyombo vya habari vya Wahouthi vimeripoti kuongezeka kwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia sehemu mbalimbali za Yemen.

Nchi hiyo imekuwa katika mgogoro tangu mwishoni mwa mwaka 2014, wakati Wahouthi walipouteka mji wa Sanaa na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, hali iliyosababisha uingiliaji wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka 2015 katika kuiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha