Watu 30 wafariki, 25 wajeruhiwa kwenye ajali ya lori kuwaka moto katika Jimbo la Giza, Misri (5)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2026
Watu 30 wafariki, 25 wajeruhiwa kwenye ajali ya lori kuwaka moto katika Jimbo la Giza, Misri
Picha hii iliyopigwa Novemba 25, 2026, ikionesha athari ya ajali ya lori kuwaka moto katika Jimbo la Giza, Misri. (Xinhua/Xin Mengchen)

CAIRO – Watu wasiopungua 30 wamefariki dunia na wengine 25 kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa limebeba bidhaa za mafuta kupata ajali na kuwaka moto jana Jumatano katika Jimbo la Giza, Misri, karibu na mji mkuu Cairo, ofisi ya mwendesha mashtaka ya umma ya nchi hiyo imesema.

Ofisi hiyo imesema katika taarifa yake kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo iliyotokea kwenye Barabara ya Mzunguko katika wilaya ya Al-Warraq, ambayo pia imeharibu kabisa vyombo vya usafiri 27, yakiwemo magari na pikipiki.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa timu za waendesha mashtaka zilitumwa kwenye eneo la tukio ili kuchunguza mazingira yaliyosababisha ajali hiyo, na kwenye hospitali za eneo hilo ili kuhoji majeruhi na kuchunguza miili ya waliofariki.

Ofisi hiyo ya mwendesha mashtaka pia imeagiza kufanywa vipimo vya vinasaba (DNA) kwenye mabaki ya waathirika wasiotambulika ili kuthibitisha utambulisho wao, ikibainisha kuwa idadi kamili ya waathirika na hasara ya mali bado ilikuwa ikifanyiwa tathmini.

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi, ametoa rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia majeruhi nafuu ya haraka, ofisi ya rais imesema katika taarifa.

Sisi pia ameelekeza mamlaka husika kutoa uungaji mkono na huduma kamili kwa majeruhi na familia za waathirika, kusafisha eneo la tukio haraka iwezekanavyo, na kuhakikisha usalama wa umma.

Waziri Mkuu wa Misri Mostafa Madbouly ameagiza kutolewa kwa huduma za matibabu, fidia kwa walioathirika, na kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu mazingira ya ajali hiyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka baraza la mawaziri.

Naye Waziri wa Mshikamano wa Kijamii wa Misri, Maya Morsy, ameelekeza kufanyika kwa uratibu na shirika la Hilali Nyekundu la Misri kwa ajili usaidizi wa ahueni katika eneo la tukio.

Wizara ya Afya wa Misri imesema katika taarifa ya awali kuwa magari ya wagonjwa 39 yalishiriki katika shughuli za uokoaji, na Waziri wa Afya, Khaled Abdel Ghaffar, alielekea hospitalini kufuatilia hali ya majeruhi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha