Afrika Kusini yazindua kampeni ya kupambana na ukatili wa kijinsia (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2026
Afrika Kusini yazindua kampeni ya kupambana na ukatili wa kijinsia
Waandamanaji wakitembea kwenye maandamano dhidi ya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake (GBVF) jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 21, 2026. (Picha na Ihsaan Haffejee/Xinhua)

JOHANNESBURG - Afrika Kusini imezindua kampeni ya siku 16 ya Uanaharakati kwa ajili ya Kutokuwa na Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto siku ya Ijumaa huku Kaimu Rais wa nchi hiyo Paul Mashatile akitoa wito wa uwajibikaji imara zaidi na hatua madhubuti za kukabiliana na ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake (GBVF).

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kitaifa iliyofanyika Middelburg katika Jimbo la Mpumalanga, Mashatile alisema kampeni hiyo lazima iende zaidi ya uhamasishaji wa umma na kuleta maboresho halisi katika usalama na ulinzi wa wanawake na watoto.

Alisisitiza kuwa kupambana na ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake kunahitaji hatua endelevu mwaka mzima badala ya kutegemea tu kampeni za uhamasishaji za mwaka na ahadi za kisera.

Kampeni hiyo ya mwaka 2026 itafanyika rasmi kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10, ikiwa na kaulimbiu isemayo: "Letsema: Wanaume, Wanawake, Wavulana na Wasichana Wanafanya Kazi Pamoja Kukomesha Ukatili wa Kijinsia na Mauaji ya Wanawake."

Mashatile alisema kuwa uzinduzi huo wa kitaifa umefanyika siku tano kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni hiyo, jambo linaloashiria uharaka wa kushughulikia tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Ili kuimarisha mwitikio wa serikali, Hazina ya Taifa ya Afrika Kusini imetenga kiasi cha ziada cha randi milioni 157.4 (dola za Marekani takriban milioni 9.1) kwa ajili ya Wizara ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, katika kipindi cha muda wa kati.

Fedha hizo zitatumika kuunga mkono uratibu na usimamizi wa kitaifa wa programu zinazohusu ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake, vilevile juhudi za kupanua mahakama, vituo vya kuhudumia waathirika, na huduma za ustawi wa jamii.

Afrika Kusini inaendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Utafiti wa kwanza wa kitaifa kuhusu ukatili wa kijinsia, uliofanywa na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu, iliyotolewa mwaka 2024, ilibaini kuwa zaidi ya mmoja kati ya kila wanawake watatu wazima nchini humo, wamewahi kukumbwa na ukatili wa kushambuliwa kimwili au wa kijinsia katika maisha yake.

Kampeni hiyo inakuja wakati kukiwa na wasiwasi mpya wa umma juu ya mauaji ya wanawake, kufuatia kubainika kwa miili ya wanawake 12 huko Ekurhuleni, mashariki mwa Johannesburg, tangu mwezi Julai

Akijibu hali hiyo, Rais Cyril Ramaphosa alitangaza hatua nne za haraka za kuingilia kati mwezi Septemba, zikiwemo: kupitia upya kesi ambazo hazijatatuliwa zinazohusu mauaji na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto; hatua za kukamilisha mlundikano wa uchunguzi wa kisayansi; ukaguzi wa usalama katika maeneo ya umma ndani ya manispaa; na hatua kali zaidi dhidi ya vurugu zinazochochewa na matumizi ya pombe.

Mashatile alisema serikali inalenga kubadili kampeni hiyo kuwa juhudi endelevu ya mwaka mzima inayohusisha sekta zote za jamii.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha