Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yafungua sehemu ya Afrika Kusini (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 20, 2026
Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yafungua sehemu ya Afrika Kusini
Balozi wa China nchini Afrika Kusini, Wu Peng, akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa sehemu ya Afrika Kusini ya Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika, jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 19, 2026. (Xinhua/Chen Wei)

JOHANNESBURG – Sehemu ya Afrika Kusini ya Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika imeanza jijini Johannesburg jana Alhamisi, huku maafisa na wawakilishi wa sekta ya biashara wa Afrika Kusini wakitoa wito wa uhusiano wa kina zaidi wa kibiashara na uwekezaji na China.

Maonesho hayo ya siku tatu, yanayofanyika sambamba na Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Viwanda ya Afrika Kusini (SAIIE), yanatoa jukwaa kwa wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili kuchunguza fursa, kuanzisha ushirikiano, na kufikia makubaliano ya kibiashara.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi, John Steenhuisen, Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushindani wa Afrika Kusini, amesema nchi hizo mbili zinashiriki maono ya kujenga ubia kwa msingi wa ushirikiano wa kina zaidi wa kiuchumi na maendeleo ya pande zote. Amehimiza wafanyabiashara kutoka pande zote mbili kutumia kikamilifu maonesho hayo ili kuchunguza fursa zilizopo.

Kampuni za Afrika Kusini jumla ya 40 na watengenezaji bidhaa zaidi ya 190 kutoka China wanashiriki kwenye maonesho hayo ya SAIIE. Maonesho hayo yanachukua eneo la mita za mraba 5,000 na yanajumuisha sehemu nne: nishati na umeme, mitambo na vipuri, madini, na bidhaa za Afrika.

China ilianza kutoza ushuru-sifuri kwa bidhaa kutoka nchi zote 53 za Afrika ambazo ina uhusiano wa kidiplomasia nazo tarehe 1 Mei.

Balozi wa China nchini Afrika Kusini, Wu Peng, amesema biashara kati ya nchi hizo mbili imekua kwa kiasi kikubwa tangu sera hiyo ilipoanza kutumika, akiongeza kuwa kampuni za China zina nia ya kuwekeza nchini Afrika Kusini na kuchangia katika maendeleo yake ya uchumi na utoaji wa ajira.

Simohn Engelbrecht, Mkuu wa Biashara na Uhusiano katika shirika la Agriculture South Africa, amesema Afrika Kusini iko katika nafasi nzuri ya kuisambazia China bidhaa mbalimbali za kilimo mwaka mzima, na inalenga kupanua wigo wa bidhaa inazouza katika soko la China.

"Kimsingi, fursa kwetu si tu kuongeza kiasi cha biashara, bali pia kujenga uhusiano wa kiuchumi ulio imara zaidi na wa mambo mbalimbali kati ya Afrika Kusini na China," amesema Engelbrecht.

Mfululizo wa vikao vya kukutanisha wafanyabiashara kujenga mitandao vikijikita katika mashine za kilimo, nishati mpya na saa pia vitafanyika wakati wa maonesho hayo ya siku tatu ili kuwezesha ushirikiano wa kibiashara na makubaliano ya biashara kati ya kampuni za China na Afrika Kusini. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha