Lugha Nyingine
Waziri wa Somalia, afisa wa Gabon waeleza matumaini makubwa juu ya CIIE huku nchi zao zikishiki kwa mara ya kwanza
SHANGHAI, China - Maafisa kutoka Somalia na Gabon wamekaribisha fursa zinazotolewa na Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE), wakielezea matumaini kwamba ushiriki kwa mara ya kwanza wa nchi zao utaimarisha uhusiano wa kibiashara, kuvutia uwekezaji na kupanua ufikiaji wa soko kubwa la China.
Akizungumza na People's Daily Online ndani ya banda la nchi yake kwenye maonesho hayo ya 9 yanayoendelea mjini Shanghai mashariki mwa China jana Alhamisi Novemba 5, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Somalia, Balozi Gamal Mohamed Hassan, ameuelezea ushiriki wa kwanza wa nchi hiyo kuwa ni hatua muhimu katika kushirikiana kiuchumi na China.
"Matarajio yetu ni makubwa sana. Hii ni mara ya kwanza Somalia kushiriki katika maonesho haya, na tunaishukuru sana serikali ya China kwa kuwezesha ushiriki wetu na kutoa fursa kwa jumuiya yetu ya wafanyabiashara kuwa hapa," amesema.
Hassan ameeleza imani kwamba maonesho hayo yatatengeneza fursa mpya kwa bidhaa za Somalia, hasa kwa kuunganisha biashara za ndani na wanunuzi wa China na kutumia sera ya ushuru-sifuri ya China kwa nchi za Afrika.
"Tunatarajia kuona fursa zaidi za biashara hapa China na kuongezeka kwa mauzo ya nje kutoka Somalia hadi China. Tukitumia manufaa yanayoletwa na sera ya ushuru-sifuri, nina matumaini makubwa," amesema.
Waziri huyo ameuelezea uhusiano wa Somalia na China kuwa bora zaidi, kisiasa na kibiashara, akibainisha kuwa China inabaki kuwa mshirika mkubwa wa biashara wa Somalia.
Huku akitambua uwepo wa muda mrefu wa wafanyabiashara wa Somalia nchini China, waziri huyo amesema nchi yake ina nia ya kupanua nafasi yake ya mauzo ya nje na kufikia uhusiano wa biashara wenye uwiano zaidi.
Kwa Gabon, kushiriki katika CIIE pia ni fursa ya kukuza uwezo wake wa viwanda na kuvutia uwekezaji, hasa katika sekta ya usindikaji wa mbao.
Roland Alfred Lendoye, Mkuu wa Uhusiano wa Wawekezaji katika Mamlaka ya Eneo Maalum la Uwekezaji la Nkok, amesema maonesho hayo yanatoa jukwaa muhimu la kuunganisha kampuni na wawekezaji.
"Fursa hii ni muhimu sana kwa sababu inaziunganisha kampuni na wawekezaji. Kuna fursa kubwa ambazo tunaweza kupata kutokana na ushiriki huu," amesema.
Lendoye amesisitiza umuhimu wa bidhaa za mbao zilizosindikwa kwa uchumi wa Gabon, akibainisha kuwa sehemu kubwa ya uzalishaji wa mbao zilizosindikwa nchini humo hutoka kwenye Eneo Maalum la Uwekezaji la Nkok.
Ameitambua China kuwa mahali pazuri pa bidhaa hizi, na kuifanya CIIE kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano wa kibiashara uliopo na kuchunguza fursa mpya.
"Matarajio yetu ni kuanzisha mitandao zaidi ya uhusiano na kuvutia wawekezaji wa ziada katika Eneo Maalum la Uwekezaji la Nkok," amesema.
Pia ametoa wito kwa wanunuzi wakubwa wa China kuchunguza fursa za kutafuta bidhaa za Gabon, hasa veneer, plywood na mbao zilizokatwa, huku akiwahimiza wawekezaji wa China kuzingatia kuanzisha biashara nchini Gabon.
Ushiriki wa Somalia na Gabon kwenye maonesho haya unaonesha juhudi zinazoongezeka za nchi za Afrika katika kuitumia CIIE kama lango la kuingia soko kubwa la watumiaji wa China, huku zikijiweka katika nafasi ya kuwa mahali pa kuvutia kwa uwekezaji wa kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




