Lugha Nyingine
Kampuni ya China yasaidia kuboresha kituo cha kwanza cha Afrika cha kuzalisha umeme kwa nishati ya jotoardhi nchini Kenya (4)
![]() |
| Picha iliyopigwa Oktoba 19, 2026 ikionesha Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Jotoardhi cha Olkaria I kwenye Hifadhi ya Taifa ya Hell's Gate katika Kaunti ya Nakuru, Kenya. (Xinhua/Xie Jianfei) |
NAIROBI – Moshi wa mvuke unapaa juu ya Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Jotoardhi cha Olkaria I, kilichopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Hell's Gate ya Kenya, wakati mabomba yakipitisha mvuke kutoka kwenye kina kirefu ardhini hadi kwenye vitengo vya kuzalisha umeme, ambako joto la ardhini hubadilishwa kuwa umeme.
Kituo hiki cha Olkaria I kilichozinduliwa rasmi katika miaka ya 1980 kama kituo cha kwanza cha Afrika cha kuzalisha umeme kwa nishati ya jotoardhi, kilikabiliwa na changamoto zilizokuwa zikidi kuongezeka katika kudumisha uwezo wake wa uzalishaji na ufanisi kwani vifaa vyake vilikuwa vimechakaa baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya miongo minne.
Kufuatia mradi wa ukarabati uliofanywa na Kampuni ya Ujenzi wa Umeme ya SEPCOIII — kampuni tanzu ya Shirika la Ujenzi wa Nishati la China — uwezo wa jumla wa uzalishaji wa kituo hicho umeongezeka kutoka megawati 45 (MW) hadi megawati 63, wakati kiasi cha mvuke kinachopatikana kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kimebakia vilevile.
Kenya, iliyo kwenye Bonde Kuu la Ufa, ina uwezekano mkubwa wa nishati ya jotoardhi. Takwimu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ya Kenya zinaonesha kuwa nishati ya jotoardhi inachukua asilimia takriban 40 ya uzalishaji wote wa umeme wa kitaifa, hali ambayo inaifanya kuwa chanzo kikuu cha umeme cha nchi hiyo.
Chini ya Mkakati wa Taifa wa Nishati wa Kenya wa 2025-2030, nchi hiyo inalenga kuongeza uwezo wake wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jotoardhi hadi kufikia megawati 1,681 (MW) ifikapo mwaka 2030, na kufikia lengo la kuzalisha umeme safi kwa asilimia 100.
"Kuboresha kituo kilichopo kunaweza kuwa na changamoto zaidi kuliko kujenga kituo kipya," amesema Zhang Yang, naibu meneja wa mradi huo wa ukarabati.
Mradi huo wa ukarabati, ulioanza mwezi Agosti 2023, ulihusisha uboreshaji wa vitengo vyote vitatu vya uzalishaji ndani ya msingi wa miundombinu ya kituo hicho ambayo ina umri wa miongo kadhaa. Zhang amesema wahandisi walilazimika kuhakikisha kuwa vifaa vipya vinaendana na mifumo iliyopo wakati huohuo wamezifanya sehemu za mitambo na umeme kufanya kazi pamoja ndani ya mpangilio wa awali wa kituo hicho.
Maurice Awuor, meneja wa uhandisi wa umeme katika Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Kenya (KenGen), amesema ukarabati huo umeongeza uwezo wa mitambo ya kituo hicho hadi Megawati 63, sawa na asilimia takriban 2 ya uwezo wote wa Kenya uliosanikiwa wa kuzalisha umeme.
"Huu ni mradi pekee wa ukarabati wa mitambo ya jotoardhi nchini Kenya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambao umezinduliwa na kuongeza uwezo uliosanikiwa kwenye gridi ya taifa," Awuor amesema.
Awuor amesema kampuni za China zina nguvu katika teknolojia na vifaa, na ushirikiano nazo ulikuwa muhimu kwa Kenya wakati huu inapojaribu kuendeleza rasilimali zake za jotoardhi.
Zhang Liang, meneja wa mradi huo, amesema baadhi ya maeneo yanayozunguka kituo hicho awali yalikumbwa na kukatika kwa umeme kwa kujirudia kutokana na uhaba wa umeme, na kwamba uwezo huo wa ziada uliosanikiwa wa Olkaria I umesaidia kuimarisha usambazaji umeme katika maeneo hayo.
Ameongeza kuwa umeme wa jotoardhi unaweza pia kuendana na vyanzo vingine vya nishati mbadala. Amesema, wakati uzalishaji wa nishati za upepo na jua hubadilikabadilika kulingana na hali ya hewa na wakati wa siku husika, vituo vya jotoardhi vinaweza kutoa usambazaji tulivu wa umeme, vikisaidia kujenga uwiano wa gridi ya taifa wakati uzalishaji wa upepo ni mdogo au uzalishaji wa nishati ya jua unapopungua baada ya jua kuzama.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




