Timu ya uokoaji ya China yabaini dalili za uhai chini ya jengo lililoporomoka jijini Nairobi, Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 29, 2026
Timu ya uokoaji ya China yabaini dalili za uhai chini ya jengo lililoporomoka jijini Nairobi, Kenya
Mtaalamu wa uokoaji kutoka China (wa pili kutoka kulia) akizungumza na mtaalamu wa Kenya kwenye eneo la jengo lililoporomoka huko Eastleigh, Nairobi, Kenya, Oktoba 27, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)

NAIROBI - Timu ya uokoaji ya China imebaini ishara za uhai chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, jambo linaloleta matumaini ya kupatikana kwa manusura wakati huu ambapo operesheni ya pamoja ya uokoaji ikiendelea, maafisa wa Kenya walisema Jumanne.

Anthony Muchiri, meneja wa operesheni za dharura katika Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na afisa anayesimamia operesheni ya shirika hilo kwenye eneo la tukio, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa wanakikundi wa Shirika la Uokoaji la Blue Sky, shirika la kibinadamu la China la uokoaji wakati wa majanga — wamebaini ishara mbili tofauti za uhai, chini kabisa ya vipande vya zege na vyuma vilivyopindika.

"Kwa kutumia vifaa maalum kutoka China, waokoaji wameweza kubainisha maeneo mahsusi ya kufanyia utafutaji, badala ya mbinu iliyotumika awali ya kuondoa vifusi katika maeneo mapana," alisema Muchiri.

Waokoaji kutoka shirika hilo la Blue Sky waliwasili kwenye eneo hilo la ajali Jumatatu wiki hii wakiwa na vifaa maalum vya kubaini uhai, ikiwemo rada zenye usahihi wa hali ya juu, vifaa vya kuhisi mitetemo na sauti, pamoja na kamera maalum zinazoweza kupenya kwenye nafasi finyu kama nyoka.

Zhang Yuran kutoka shirika hilo la Blue Sky amesema kuwa timu hiyo imekuwa ikifanya kazi ya kutafuta watu walio hai na kushirikiana na timu nyingine kadhaa za uokoaji zilizopo kwenye eneo la tukio.

Ameongeza kuwa waokoaji wameanza kufungua njia za kufikia maeneo hayo mawili ambako ishara za uhai zilibainiwa.

Mashine zilizotolewa na kampuni za China pia zimeunga mkono operesheni hiyo ya uokoaji.

William Sifuna Watitwa, afisa mfanyakazi katika eneo la kaskazini la Nairobi, amesema kuwa Kampuni ya Mashine za Ujenzi ya Xuzhou ya China imetoa mashine ya kuchimba (excavator) na kreni ya tani 25 ili kusaidia juhudi za utafutaji.

"Mashine hii ya kuchimba ilitoa mchango mkubwa katika kuokoa watu wawili waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi siku ya Jumamosi," amesema Watitwa.

Jengo hilo la ghorofa nyingi liliporomoka Ijumaa huko Eastleigh, eneo lenye msongamano mkubwa wa shughuli za biashara na makazi jijini Nairobi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha