Lugha Nyingine
Lula ashinda uchaguzi wa rais wa Brazil; Bolsonaro akataa kisha akubali kushindwa huku akipigwa marufuku kusafiri nje (2)
BRASILIA – Rais aliyeko madarakani sasa wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, mgombea wa chama tawala cha Workers' Party, ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais iliyofanyika Jumapili, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Mahakama ya Juu ya Uchaguzi ya Brazil usiku wa Jumapili.
Huku asilimia 99.99 ya kura zikiwa zimehesabiwa, Lula alipata asilimia 51.79 ya kura zote halali zilizopigwa, ikilinganishwa na asilimia 48.21 alizopata Flavio, mgombea urais wa chama cha Liberal Party na mtoto wa rais wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro, kwa mujibu wa hesabu rasmi.
Lula ataapishwa Januari 5, 2027, kwa muhula wa miaka minne, ambao utakuwa muhula wake wa nne kuwa rais wa Brazil.
Akizungumza katika hotuba ya moja kwa moja jijini Sao Paulo kufuatia ushindi wake, Lula ameahidi kushirikiana na Bunge lenye mwelekeo wa kihafidhina lililochaguliwa na wananchi, na kuhakikisha ushiriki mpana zaidi wa umma katika mchakato wa kufanya maamuzi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa masuala ya kidijitali baada ya kuushinda uingiliaji wa nje kupitia majukwaa ya kidijitali, akisisitiza kuwa Brazil si "yadi ya nyuma" ya nchi nyingine yoyote.
Lula pia ameahidi kuimarisha huduma za afya kwa umma, kuboresha huduma kwa wazee, kuheshimu wanawake, na kuendeleza juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakati huo huo, Flavio Bolsonaro, akizungumza katika mji mkuu wa Brazil, Brasilia siku hiyo ya Jumapili, alisema "haiwezekani" kukubali matokeo hayo, na akatoa wito wa kufutwa kwa uchaguzi huo, akidai kutendewa kusiko sawa kwa wapiga kura kufuatia uamuzi wa kuongeza muda wa kupiga kura.
Hata hivyo baadaye jana Jumatatu Chama chake cha Liberal, kilikubali matokeo hayo, kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama hicho, Valdemar Costa Neto.
Tangazo hilo lilikuja baada ya wajumbe wa kampeni ya Bolsonaro kukiambia kituo cha utangazaji cha CNN Brazil kwamba ameamua kutotafuta kufutwa kwa matokeo hayo ya duru ya pili, na badala yake atachukua hatua za kisheria juu ya madai ya matumizi mabaya ya madaraka ya kisiasa na kiuchumi yaliyofanywa na kambi ya kampeni ya Rais Lula da Silva.
Katika hatua nyingine, Jaji wa Mahakama Kuu ya Serikali Kuu ya Brazil, Alexandre de Moraes, ameamuru mgombea huyo urais aliyeshindwa, Flavio Bolsonaro, akabidhi pasipoti zake kwa Polisi wa Serikali Kuu na kumzuia kuondoka nchini humo, vyombo vya habari vya Brazil vimeripoti jana Jumatatu.
Uamuzi huo wa siri, ni sehemu ya uchunguzi unaomhusisha Bolsonaro na mwanasheria Willer Tomaz, kwa mujibu wa shirika la habari la umma la Brazil, Agencia Brasil.
Vyombo vya habari vya Brazil vimeripoti kuwa Moraes pia amemkataza Bolsonaro kuwasiliana na Tomaz. Wote wawili wako chini ya uchunguzi wa Polisi wa Serikali Kuu kwa tuhuma za utakatishaji fedha na miamala haramu ya fedha za kigeni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




