Lugha Nyingine
Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Anga ya Juu wafunguliwa Paris huku Marekani ikikosekana (3)
![]() |
| Kifaa kikioneshwa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Anga ya Juu katika Grand Palais jijini Paris, Ufaransa, Septemba 9, 2026. (Xinhua/Wu Huiwo) |
PARIS - Mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa Anga ya Juu umefunguliwa rasmi jana Jumatano mjini Paris, Ufaransa ukiwaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali, wanasayansi, wanaanga na wawakilishi wa tasnia hiyo.
Mkutano huo wa siku mbili ulioanzishwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na kuandaliwa kwa pamoja na Ufaransa na Ujerumani, unatarajiwa kuvutia washiriki wapatao 2,000.
Majadiliano kwenye mkutano huo yatajikita katika sayansi na uchunguzi wa anga ya juu, ikiwemo uchunguzi wa sayari ya Mirihi, uchunguzi wa bahari na utafiti wa anga ya juu; uchumi wa anga ya juu duniani, ikiwemo ufikiaji wa anga ya juu, muunganisho, mambo ya viwanda na uwezo wa ushindani wa Ulaya; na usalama na usimamizi wa anga ya juu.
Hata hivyo, mkutano huo ulikuwa umefunikwa na mivutano ya nchi za pande za Atlantiki kabla ya kufunguliwa kwake, huku kampuni kubwa za anga ya juu za Marekani zikifuta ushiriki wao. Gazeti la kila siku la Ufaransa, Le Monde, limeripoti kwamba kampuni hizo kubwa za anga ya juu, Blue Origin na SpaceX, vilevile Stoke Space na Starcloud, zilijiondoa kwenye mkutano huo.
Chombo cha habari cha Politico awali kiliripoti kwamba Ikulu ya Marekani ilikuwa imezishinikiza kampuni za anga ya juu za Marekani kuachana na mkutano huo kwa madai kwamba mahudhurio yao yanaweza kuonekana kama uungaji mkono kimyakimya kwa misimamo ya sera za Umoja wa Ulaya (EU).
Xavier Pasco, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kimkakati, alisema Jumatano kwenye mahojiano na shirika la umma la utangazaji la Ubelgiji, RTBF kwamba kutokuwepo kwa kampuni kubwa za Marekani kumehamasishwa kisiasa, wakati huu ambapo EU inaandaa Sheria yake ya Anga ya Juu. Sheria hiyo mpya itaweka mfumokazi wa usimamizi wa shughuli za anga ya juu, na Marekani pia inataka kuwa na kauli kwenye sheria hiyo mpya.
"Kwa hiyo kuna upande wa mtafaruku wa kiishara," Pasco alisema.
Aidha, mkutano huo pia umeshuhudia kutohudhuria kwa Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ambaye alikuwa amepangwa kuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo na Macron. Kituo cha habari cha Ufaransa, BFM TV, kikimrejelea msemaji wa serikali ya Ujerumani, kimeripoti kwamba ratiba yenye shughuli nyingi ya Merz imemwacha "bila nafasi" ya kuhudhuria.
Kwa mujibu wa gazeti la Le Monde, sehemu inayohusiana na anga ya juu ya euro takriban bilioni 60 (dola bilioni 69.78 za Marekani) inapaswa kujumuishwa kwenye mfumokazi ujao wa kifedha wa EU wa 2028-2034. Wakati Ufaransa inataka ufadhili huo uambatane na upendeleo kwa Ulaya katika manunuzi na vigezo vingine, Ujerumani inapinga baadhi ya mapendekezo hayo na inataka kampuni zake mpya kuwa na kujitegemea na uhuru.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




