Canada yatangaza ushuru wa kulipiza kwa bidhaa zaidi ya 700 za Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 26, 2026
Canada yatangaza ushuru wa kulipiza kwa bidhaa zaidi ya 700 za Marekani
Magogo ya mbao yakionekana yakielea kwenye Mto Fraser, Vancouver, British Columbia, Canada, Agosti 25, 2026. (Picha na Liang Sen/Xinhua)

OTTAWA - Serikali Kuu ya Canada imetangaza ushuru wa kulipiza kwa bidhaa zaidi ya 700 za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 27.6 za Canada (dola karibu bilioni 20 za Marekani), pamoja na kifurushi cha usaidizi cha dola bilioni 7.5 za Canada kwa biashara na wafanyakazi wa ndani.

Maafisa wa Canada wamesema jana Jumanne kwamba hatua hizo za kulipiza zinalingana na thamani ya jumla ya bidhaa za Canada zilizolengwa na ushuru wa hivi karibuni wa asilimia 50 wa Marekani, hali inayotimiza jibu la "dola kwa dola, kiwango kwa kiwango". Ushuru huo wa kulipiza umepangwa kuanza kutumika rasmi Septemba 8.

Waziri wa Fedha wa Canada Francois-Philippe Champagne amesema ushuru huo wa kulipiza vilevile kifurushi hicho cha kuunga mkono cha mabilioni ya dola vitalinda wafanyakazi, wakulima, familia na biashara.

Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Canada, ushuru huo mpya wa kulipiza wenye lengo mahsusi unajikita zaidi katika sekta kama vile chuma, maziwa, vifaa vya umeme, vifaa vya kilimo, massa na karatasi, na vifaa vya kielektroniki, huku viwango hivyo vya ushuru vikiwa katika ngazi tatu: asilimia 15, asilimia 25 na asilimia 50.

Wizara hiyo imesema, katika sekta kadhaa, kama vile chuma na aluminiamu, ushuru uliopo utaongezeka kutoka asilimia 25 hadi asilimia 50 ili kuendana na viwango vya Marekani. Imesema, shuru mwingine wa kulipiza uliopo, ukiwemo ule wa dhidi ya magari ya Marekani, pia utaendelea kutumika.

Imesema kwamba ushuru wa asilimia 25 utatozwa kwa bidhaa za maziwa kama vile jibini, samaki, vyakula vya baharini, na bidhaa zinazotokana na chuma na aluminiamu.

Mbali na ushuru huo, serikali kuu hiyo ya Canada imetangaza kifurushi cha unafuu chenye thamani ya dola bilioni 7.5 za Canada, hasa kikilenga biashara zenye ukubwa mdogo na wa kati. Ottawa pia imeahidi kuzisaidia kampuni kuepuka kupunguza wafanyakazi, kuwezesha wafanyakazi zaidi kuboresha ujuzi, na kuongeza unyumbulifu wa kupata bima ya ajira.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha