Lugha Nyingine
Kampuni za China zapanua njia ya kufikia elimu kwa watoto wa vijijini nchini Zambia (2)
LUSAKA - Mirriam Chola, mwanafunzi katika Jimbo la Copperbelt la Zambia, kwa muda mrefu alikuwa akiota kuhudhuria shule ambayo anaweza kufika kwa kutembea kwa miguu kutoka nyumbani kwake huko Kalulushi, mji wa pembezoni karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Nilikuwa nikisoma katika shule ya Katoliki ambapo nilikuwa na changamoto ya kuwa pamoja na familia yangu, na nilikuwa nikiwakumbuka sana," Chola amekumbushia. Amesema ilibidi akosekane kwenye mijumuiko mingi ya kifamilia wakati akifuatilia masomo katika mji ulio mbali na nyumbani.
Ndoto hiyo ya Chola hatimaye ilitimia mwaka 2025 wakati Kampuni ya Sino-Metals Leach Tawi la Zambia (SMLZL), kampuni ya uchimbaji madini ya China, iliposaidia kujenga Shule ya Sekondari ya Minsenga katika mji wa asili yake.
Akiwa ameketi ndani ya darasa kubwa lenye mwanga mzuri lililo na vifaa vipya na vya kisasa, Chola anahisi furaha sana.
"Ninafika shuleni mapema, nikijipa muda wa kupumzika na kutuliza akili yangu ili niweze kujifunza mambo mapya zaidi," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, akiongeza kuwa anajitahidi kwa moyo wote kupata udahili katika chuo kikuu na kuwa mhandisi katika siku zijazo.
Nchini Zambia, wanafunzi wengi katika maeneo ya vijijini wana changamoto za kupata elimu kutokana na ukosefu wa shule, walimu, na vifaa vya kujifunzia, hali inayosababisha baadhi kuacha shule wakiwa na umri mdogo.
Wakati huu ambapo serikali ya Zambia ikijitahidi kuboresha elimu ya vijijini, idadi inayozidi kuongezeka ya kampuni za China zinazofanya shughuli zao nchini Zambia zimejiunga na juhudi hizo kwa kujenga miundombinu ya shule na kuchangia vifaa vya kielimu, hali ambayo imesaidia watoto wengi kupata ufikiaji wa elimu.
Andrew Mfune, mkuu wa Shule ya Sekondari ya Minsenga, ameliambia Xinhua kwamba SMLZL si tu imejenga vyumba vya madarasa na kutoa vifaa vya steshenari kwa wanafunzi, lakini pia imerejesha matumaini yao ya siku zijazo.
"Wengi wao walichagua kuacha shule kwa sababu hawakuwa na chaguo lingine, na mustakabali wao uliharibika," Mfune amesema. "Lakini sasa wanafunzi wote walio karibu wanaweza kuendelea na elimu yao ya sekondari."
Mfune amesifu mchango chanya ambao kampuni za China zimetoa katika kuchochea elimu ya vijijini ya Zambia, akisema ishara hizo pia zimeimarisha urafiki wa kudumu kati ya watu wa Zambia na China.
Kwa mujibu wa Sydney Chileya, naibu afisa mtendaji mkuu wa SMLZL, uungaji mkono wa kila mara wa kampuni hiyo kwa elimu katika maeneo ya vijijini unaendana na sera ya serikali ya Zambia ya kuwekeza katika mustakabali wa muda mrefu wa nchi hiyo, huku elimu ikiwa moja ya nguzo zake.
"Tumeunga mkono shule zingine kadhaa, miongoni mwao Shule ya Sekondari ya Chambishi, ambayo tuliifanyia ukarabati na pia kununua madawati kwa ajili ya watoto kukaa," amesema Chileya, akiongeza kuwa juhudi hizo zimeongeza udahili wa shule miongoni mwa watoto kutoka familia zisizojiweza katika jamii za karibu.
Kwa kutoa uungaji mkono unaohitajika sana kwa shule zinazokabiliwa na vizuizi vya kifedha na changamoto zingine, Chileya amesema, kampuni hiyo inalenga kutengeneza fursa kwa wanafunzi kufuata ndoto zao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




