Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China katika nusu ya kwanza ya mwaka yarekodi ukuaji wa asilimia 16.9 (2)
![]() |
| Picha iliyopigwa Julai 14, 2026 ikionyesha mwonekano wa gati la kimataifa la makontena kwenye Bandari ya Yantai katika Mkoa wa Shandong, mashariki mwa China. (Picha na Tang Ke/Xinhua) |
BEIJING - Biashara ya nje ya China imeongezeka kwa asilimia 16.9 kutoka mwaka jana katika nusu ya kwanza ya 2026 (H1) hadi kufikia yuan trilioni 25.47 (dola za Marekani karibu trilioni 3.75), ikiashiria mara ya kwanza kwa takwimu hizo kuzidi yuan trilioni 25 kwa kipindi sawa na hicho, takwimu rasmi zilizotolewa jana Jumanne na Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) zimeonyesha.
Kwa mujibu wa GAC China inadumisha nafasi yake ya kuwa mfanyabiashara mkubwa zaidi wa bidhaa duniani huku ikiwa na ufanisi mzuri.
Kati ya jumla hiyo, mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 13.4 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho hadi kufikia yuan trilioni 14.73, yakidumisha ukuaji kwa robo 11 mfululizo, wakati huoho uagizaji bidhaa kutoka nje uliongezeka kwa asilimia 22.1 hadi kufikia yuan trilioni 10.74, asilimia ya pointi 8.7 zaidi ya kiwango cha ukuaji wa mauzo ya nje, na kuwezesha maendeleo ya biashara yenye uwiano.
Kwa mujibu wa GAC katika nusu hiyo ya kwanza, kiasi cha uagizaji kwa wingi bidhaa zisizofungashwa, zikiwemo za nishati na madini ya chuma, kiliongezeka kwa asilimia 3.4, uagizaji wa bidhaa za mitambo na umeme uliongezeka kwa asilimia 28, na uagizaji wa bidhaa za kilimo uliongezeka kwa asilimia 8.6.
"Biashara ya nje ya China imedumisha kasi nzuri katika nusu ya kwanza, ikiwa na ukuaji imara na uendeshaji tulivu, na upigaji hatua kubwa umepatikana katika kutuliza kiwango na kuboresha muundo," amesema Wang Jun, naibu mkuu wa GAC, kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China jana Jumanne.
Katika robo ya pili mwaka huu, jumla ya biashara ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ilifikia yuan trilioni 13.61, ongezeko la asilimia 18.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, na kiwango cha juu zaidi cha ukuaji kwa robo mwaka tangu robo ya tatu ya mwaka 2021. Thamani ya biashara mwezi Juni pekee iliongezeka kwa asilimia 24.2 kutoka kipindi kama hicho mwaka jana, ikifikisha ukuaji wa miezi 17 mfululizo.
Biashara na nchi zinazoshiriki katika Ukanda Mmoja, Njia Moja iliongezeka kwa asilimia 14.8 hadi kufikia yuan trilioni 12.97 katika nusu ya kwanza, ikichukua asilimia 50.9 ya jumla ya biashara ya nje. Biashara na nchi jirani iliongezeka kwa asilimia 20.6, wakati huohuo biashara na Latini Amerika, Afrika na EU ilirekodi ukuaji wa asilimia 16.2, asilimia 19.6 na asilimia 10.2 mtawalia. Biashara na nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki pia ilikua kwa asilimia 11 katika nusu ya kwanza, ikiendeleza ukuaji kwa miaka 10 mfululizo.
Lyu Daliang, mkurugenzi wa Idara ya Takwimu na Uchambuzi ya GAC, amebainisha kuwa China kwa muda mrefu imekuwa ikishikilia nafasi ya muuzaji nje mkubwa zaidi wa bidhaa za michezo duniani, ikichukua asilimia zaidi ya 40 ya mauzo yote ya nje duniani, na bidhaa nyingi za China zimeonekana kwenye Kombe la Dunia la FIFA la 2026 linaloendelea. Amesema katika nusu ya kwanza ya 2026, mauzo ya nje ya bidhaa na vifaa vya michezo ya China yalifikia yuan bilioni 67.53, miongoni mwa hayo mauzo ya nje ya mipira yalifikia yuan bilioni 3.08.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




