Upasuaji wa kuokoa maisha Zanzibar waakisi ushirikiano unaokua wa afya kati ya China na Tanzania (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 07, 2026
Upasuaji wa kuokoa maisha Zanzibar waakisi ushirikiano unaokua wa afya kati ya China na Tanzania
Daktari mchina bingwa wa mfumo wa mkojo Wang Kunpeng (wa kwanza, kulia) akifanya kazi na wafanyakazi wa matibabu wenyeji wakati wa upasuaji katika Hospitali ya Lumumba, Zanzibar, Tanzania, Januari 22, 2026. (Kundi la 35 la Timu ya madaktari Wachina visiwani Zanzibar/kupitia Xinhua)

ZANZIBAR, Tanzania - Kwa miaka mitano, Selemani Juma Selemani Mtanzania mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akiishi na hali ya maumivu, homa, na kukosa utulivu kwa kudumu kutokana na hali ngumu ya mfumo wa mkojo ambayo imekuwa ikimsumbua maisha yake ya kila siku.

Akiwa ni mfanyakazi wa hoteli katika Kisiwa cha Unguja, Zanzibar, Tanzania, Selemani alikuwa akihangaika kudumisha utaratibu wa kawaida. Wakati mwingine, hata alipunguza unywaji wake wa maji kwa kuhofia kuzifanya dalili zake kuwa mbaya zaidi.

Utaratibu huo wa muda mrefu ulifikia mwisho hivi karibuni, alipofanyiwa upasuaji mgumu wa saa tatu na nusu katika Hospitali ya Lumumba visiwani Zanzibar, uliofanywa na daktari mchina bingwa wa mfumo wa mkojo Wang Kunpeng. Ndani ya saa kadhaa, mgonjwa huyo kijana alikuwa huru kutoka kwenye mzigo wa kiafya wa miaka mingi.

"Nimekuwa nikiteseka kwa miaka mitano, lakini daktari amenitibu ndani ya saa nne," Selemani amesema baada ya upasuaji huo. "Sitamsahau kamwe daktari Mchina kwa kuokoa maisha yangu."

Hali hiyo ya Selemani ilianzia kwenye upasuaji wa awali katika hospitali ya visiwani humo, ambapo tyubu ya kupitisha haja ndogo (ureteral stent) iliachwa bila kukusudia ndani ya mwili wake. Baada ya muda, hali hiyo ilisababisha maambukizi ya mara kwa mara na kuunda mawe kadhaa kwenye figo, urethra, na kibofu, na kufanya tatizo lake kuwa gumu na kuhitaji matibabu ya haraka.

Baada ya kutafuta msaada katika Hospitali ya Lumumba, matokeo ya vipimo yalithibitisha tatizo kubwa la hali yake. Wang, mjumbe wa kundi la 35 la timu ya madaktari Wachina visiwani Zanzibar, alifanya kazi kwa karibu na mtaalamu mwenyeji wa mfumo wa mkojo Hassan Mkoko ili kutathmini tatizo hilo na kutengeneza mpango wa matibabu. Kwanza walituliza hali ya mgonjwa kupitia tiba ya kuzuia maambukizi kabla ya kuendelea na upasuaji.

Upasuaji huo ulijumuisha mbinu kadhaa za hali ya juu, ikiwemo transurethral lithotripsy ili kugawanya mawe ya kibofu, uondoaji wa tyubu hiyo iliyokuwa imeachwa mwilini, ureteroscopy, uwekaji wa tyubu mpya, na, hatimaye, upasuaji wa kuondoa mawe ya figo.

"Upasuaji ulihitaji usahihi na uratibu makini, hasa kutokana na matatizo ya awali ya mgonjwa," amesema Wang.

Upasuaji huo ulikamilika kwa upotevu wa damu chache, na dalili muhimu za mgonjwa huyo zilibaki imara katika kipindi chote. Muda mfupi baadaye, Selemani alianza kupona.

"Ninahisi nafuu zaidi sasa," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua, akiongeza kuwa anatarajia kurudia maisha na kazi yake ya kawaida.

Upasuaji huu wenye mafanikio unaakisi mchango unaozidi kuongezeka wa timu za madaktari Wachina visiwani Zanzibar na kote Tanzania. Tangu kuwasili kwao, kundi hilo la 35 la timu ya madaktari Wachina limeshatoa huduma za kliniki wakati huohuo likiweka mkazo katika uhamishaji ujuzi, matengenezo ya vifaa, na ujengaji uwezo ndani ya mifumo ya afya ya Zanzibar.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha