Lugha Nyingine
Unasihi mtambuka wa kampuni ya China waongeza ufanisi wa mradi wa miundombinu nchini Ghana (2)
ACCRA – Tangu utotoni, Eric Ampadu alikuwa akiota kufanya kazi katika nyanja ya teknolojia. Ndoto hiyo ilikaribia uhalisia alipopata udahili katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Accra mjini Accra, mji mkuu wa Ghana.
Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu mwaka 2022, Ampadu alikabiliwa na changamoto ya kupata kazi katika mazingira magumu ya soko la ajira, ambapo asilimia 32.8 ya Waghana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hawakuwa na ajira mwaka 2021, kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Ghana.
Mwezi Januari 2025, rafiki yake alimwambia kuhusu kampuni ya uhandisi inayoajiri wahitimu wa uhandisi wa ujenzi kwa ajili ya mradi.
"Niliomba kazi hiyo na niliitwa kwa ajili ya usaili. Kampuni hiyo kumbe ilikuwa Kampuni No. 5 ya Uhandisi (CR5) ya Kundi la Shirika la Reli la China Tawi la Ghana. Baada ya usaili, niliajiriwa kuwa mhandisi wa ujenzi kwenye sehemu mahsusi ya maabara kwa ajili ya majaribio ya nyenzo," kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Kazini, Ampadu amekuwa chini ya uangalizi wa Zhang Zeyun, mhandisi wa nyenzo katika CR5 Tawi la Ghana, kampuni ya uhandisi ya China inayofanya kazi ya uendelezaji na upanuzi wa Barabara Kuu ya Accra-Tema, iliyokamilishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1965 chini ya rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah.
Ameelezea uzoefu wake wa kufanya kazi na Zhang kuwa wenye manufaa makubwa, akisema anajihisi mwenye bahati kujifunza kutoka kwa mhandisi huyo mwenye uzoefu na azma. "Chini ya mwongozo wake, nimeboresha ujuzi wangu kwa kiasi kikubwa katika majaribio ya nyenzo, utendaji wa kitaalamu, na utenda kazi ulio sanifu," amesema fundi huyo kijana wa maabara.
Kwa mujibu wa mnasihi wake Zhang, Ampadu amekuwa na ufanisi katika majaribio ya maabara kwa kampuni kupitia kufanya kazi kwa bidii, kufuata maelekezo, na nia ya kujifunza kwa haraka.
Wang Su, mhandisi kijana wa kike wa Mchina ambaye amebadilikia vizuri kuzoea mazingira mapya ya kazi kupitia unasihi, ni mfano mmoja wa namna kama hiyo.
Mnasihi wake, Benedict Anane kutoka idara ya usimamizi wa rasilimali watu ya CR5 Tawi la Ghana, amekumbushia hisia zake za kwanza wakati Wang alipowasili.
"Wang alipowasili kwa mara ya kwanza, kama ilivyo kwa wataalamu wengi wanaofanya kazi katika mazingira mapya, alikabiliwa na changamoto ya mawasiliano. Lakini kinachomtofautisha ni uwazi wake wa kujifunza zaidi ya kazi ya kiufundi," amesema.
Kwa mujibu wa Anane, Wang ameonyesha shauku kubwa ya kuelewa watu, kuheshimu mila za wenyeji, na kujenga uhusiano halisia.
Chen Zhen, naibu mkurugenzi mkuu wa CR5 Tawi la Ghana, amesisitiza umuhimu wa uhusiano imara kati ya wafanyakazi wenyeji na wenzao wa China katika kuhakikisha ufanyaji kazi kwa ubora na ufanisi kwa ujumla.
"Tunafanya kazi kama timu moja jumuishi," amesema. "Tunahimiza mawasiliano ya wazi na kuheshimiana ili wafanyakazi wa China na wafanyakazi wenyeji waweze kufanya kazi pamoja katika mazingira ya kazi yenye kuishi sawa kwa mapatano."
Jitihada hizi zinatumikia lengo la pamoja linalozidi uhusiano wa kawaida wa mwajiri na mwajiriwa "na kukuza jumuiya ya maendeleo iliyojengwa juu ya kuaminiana, kubadilishana maarifa, na mapatano ya kitamaduni," ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




