

Lugha Nyingine
Kituo cha Usimamizi wa Uchukuzi Bidhaa za Biashara ya Kuvuka Mpaka cha Shenzhen, China: "Kituo cha Kisasa" nyuma ya ufanisi wa kupita forodha
![]() |
Ndani ya Kituo cha Usimamizi wa Uchukuzi Bidhaa za Biashara ya Kuvuka Mpaka cha Shenzhen. (Picha na Zhao Jian, People's Daily Online) |
Kikishughulikia wastani wa vifurushi zaidi ya 700,000 na magari zaidi ya 400 kwa siku, Kituo cha Usimamizi wa Uchukuzi Bidhaa za Biashara ya Kuvuka Mpaka cha Shenzhen, kinachopatikana Qianhai, mjini Shenzhen, China ni nguzo muhimu kwa biashara ya kuvuka mpaka ya Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao.
Wakati waandishi wa habari wa timu ya "Kufanya Utafiti kuhusu Shenzhen" ya People's Daily Online ilipowasili katika Kituo hicho, malori yalikuwa yakipita kwa utaratibu, mistari kadhaa ya uchambuzi na upangaji vifurushi kwa kutumia AI ilikuwa ikifanya kazi kwa ufanisi, na vifurushi vilikuwa vikihamishwa haraka huko.
Kampuni ya Kituo cha Usimamizi wa Uchukuzi Bidhaa za Biashara ya Kuvuka Mpaka ya Shenzhen Ilianzishwa Mei 2019 na ni kampuni tanzu inayomilikiwa kikamilifu na Kampuni ya Shenzhen Creation Group. Ina stesheni ya usimamizi yenye ukubwa wa mita za mraba karibu 25,000, huku eneo la ujenzi likiwa na mita 6,461 za mraba.
Kikiwa ni kituo muhimu kwa biashara ya kuvuka mpaka, kituo hicho kila mwaka kwa wastani kinakagua na kupitisha magari zaidi ya 100,000 ya kuvuka mipaka, na thamani ya bidhaa zinazouzwa nje kwa mwaka inazidi Yuan bilioni 200, huku uzito wa vifurushi vya bidhaa zinazouzwa nje ukizidi tani 600,000. Kituo hicho kimehuhudumia kampuni zaidi ya 50 za uchukuzi wa kuvuka mpaka na kampuni 350 za biashara ya mtandaoni ya kuvuka mpaka.
Kuanzia mfumo wa kuchambua na kupanga vifurushi kiotomatiki hadi mchakato wa usimamizi wa kutumia AI, kituo hicho kimeanzisha kwa mafanikio huduma nyingi muhimu za vifurushi kupita forodha, kama vile uuzaji bidhaa nje, uagizaji bidhaa na urejeshaji bidhaa katika biashara ya kuvuka mpaka ya mtandaoni.
Kupitia mifumo vumbuzi kama vile "kagua kwanza kisha pakia", kimetatua tatizo gumu la kufuata taratibu za utoaji vibali vya forodha chini ya aina mbalimbali za biashara.
Kwa mujibu wa Zheng Dang, naibu meneja mkuu wa kituo hicho, bidhaa za biashara ya mtandaoni ya kuvuka mipaka zinaweza kufika katika Bandari ya Ghuba ya Shenzhen ndani ya dakika 15 baada ya kupata kibali cha forodha katika kituo hicho, na zinaweza kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Hong Kong ndani ya dakika 30 kwa ajili ya kupakiwa kwenye ndege na kusafirishwa kuuzwa nje.
Amesema kituo hicho cha huduma zote katika sehemu moja kinaboresha sana urahisi wa biashara ya kuvuka mpaka na kinapunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni.
Kutokana na ujenzi wa Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao unaoendelea kwa kina, "vituo vya kisasa" kama kituo hicho vitakuwa na jukumu muhimu zaidi na kuwa nguzo muhimu kwa China kuunganisha soko la kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma