Lugha Nyingine
ChinaVumbuzi | Meli kubwa zaidi ya kubeba magari duniani yakabidhiwa nchini China, ikiongeza uwezo wa usafirishaji wa magari duniani
![]() |
| Wageni wakipiga picha ya pamoja kwenye hafla ya kukabidhi meli ya kubeba magari Glovis Leader, mjini Guangzhou, mkoani Guangdong, kusini mwa China, Aprili 28, 2026. (Xinhua/Wu Lu) |
GUANGZHOU – Meli ya kubeba magari yenye uwezo wa juu wa kubeba magari 10,800 ya kiwango sawa, inayotajwa kuwa kubwa zaidi duniani ya aina yake, ilikabidhiwa rasmi Jumanne katika Mji wa Guangzhou kusini mwa China ambapo meli hiyo, inayoitwa Glovis Leader, ilijengwa na Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Meli ya Guangzhou chini ya Shirika la Ujenzi wa Meli la China (CSSC), kwa kushirikiana na Kampuni ya Biashara ya Ujenzi wa Meli ya China.
Imekabidhiwa kwa HMM, kampuni inayoongoza ya usafirishaji wa majini katika nchi ya Korea Kusini. Baada ya kukabidhiwa, meli hiyo itaendeshwa na Hyundai Glovis, kampuni ya usafirishaji ambayo pia ina makao yake nchini humo.
Lee Kyoo-bok, Mkurugenzi Mtendaji wa Hyundai Glovis, amesema katika hafla ya makabidhiano kwamba meli hiyo kubwa sana ya kizazi kipya ni zaidi ya chombo cha kawaida cha usafiri. Amesema, kwa uwezo wake mkubwa na mfumo ulioboreshwa wa uendeshaji wa kijani, inatarajiwa kuweka kiwango kipya kwa usafirishaji wa magari baharini duniani na inaashiria hatua muhimu katika sekta ya usafirishaji majini.
Ikiwa imeainishwa kama meli maalumu ya kubeba magari na malori, meli hiyo ina urefu wa mita 230 na upana wa mita 40, ikiwa na kina cha muundo cha mita 10.5 na kasi ya safari ya noti 19. Ina deki 14 za magari na inaweza kubeba mizigo mbalimbali, ikiwemo magari yanayotumia umeme, magari yanayotumia hidrojeni na malori mazito.
Glovis Leader inaendeshwa na mfumo wa matumizi ya nishati mbili unaotumia gesi asilia ya kimiminika na mafuta ya kawaida, ikikidhi viwango vya Daraja la III vya utoaji hewa chafu vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini. Pia inajumuisha teknolojia za kuokoa nishati, zikiwemo muundo ulioboreshwa wa ganda la meli, mifumo ya kurejesha joto taka na uwezo wa kutumia umeme ufukweni.
Zhou Xuhui, meneja mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Meli ya Guangzhou, amesema kampuni hiyo imeshinda changamoto kadhaa muhimu za kiufundi kupitia ujenzi wa meli hizi kwa mfululizo wakati huohuo ufanisi wa uzalishaji pia umeimarika kwa kiasi kikubwa.
Wataalamu wa tasnia hiyo wanasema kukabidhiwa huko kwa meli hiyo kunaonyesha uwezo unaozidi kukua wa China katika ujenzi wa meli za kiwango cha juu na unaakisi juhudi pana zaidi za tasnia ya usafirishaji wa majini duniani katika kusonga mbele kuelekea uendeshaji wa utoaji mdogo wa kaboni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




