Lugha Nyingine
FAW-Volkswagen yasherehekea kufikisha gari la milioni 30 huku imani ya soko la magari ya China ikiongezeka (2)
CHANGCHUN – Wakati gari jipya aina ya Audi sedan A5L lilipokuwa likiendeshwa taratibu kutoka kwenye mstari wa uundaji magari wa kiwanda cha FAW-Volkswagen cha Changchun katika Mkoa wa Jilin wa China jana Alhamisi usiku, kampuni hiyo ya ubia imesherehekea hatua muhimu ya kihistoria -- gari lake la milioni 30 lililoundwa nchini China.
Ralf Brandstätter, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kampuni za Volkswagen Tawi la China, ameuita wakati huo hatua muhimu, akiuelezea kuwa ni "ishara ya kufanya kazi kwa ushirikiano, kuaminiana na uhusiano imara wa kiwenzi kati ya FAW na Volkswagen."
Hatua hiyo muhimu si tu kwa ajili ya kampuni moja, bali ni ishara kali kwa waundaji magari duniani kwamba likiwa ni soko kubwa zaidi la magari duniani, China ni fursa isiyoweza kukoswa kwa kampuni za duniani zenye nia kubwa.
Ikiwa ilianzishwa mwaka 1991, kampuni hiyo ya ubia ya FAW-Volkswagen imekua kutoka kuzalisha aina moja ya gari la Jetta chini ya chapa moja hadi kuzalisha aina 33 za magari yanayotumia mafuta na nishati mpya (NEVs).
Shughuli zake sasa zinajumuisha viwanda sita katika miji mitano, ambayo ni Changchun, Chengdu, Foshan, Qingdao na Tianjin. Katika miaka zaidi ya 34 iliyopita, kampuni hiyo imerekodi mapato ya jumla yanayozidi yuan trilioni 5.5 (Dola za Kimarekani karibu bilioni 776).
"China na Ujerumani zina moja ya uhusiano wa kiwenzi wa kiviwanda unaoaminika na wenye mafanikio zaidi duniani. Kampuni yetu ni mfano mzuri wa hili," Brandstätter amesema.
Huku China ikiendelea kufungua mlango wake kwa upana zaidi, mchanganyiko wake wa uungaji mkono wa kisera, uvumbuzi, na mahitaji makubwa ya wanunuzi unawapa waundaji magari duniani sababu mpya za kubaki na kukua nchini humo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Biashara wa China Wang Wentao, China ilivutia dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 720 katika uwekezaji wa kigeni wakati wa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025), huku zaidi ya theluthi moja ya uwekezaji huo ukiingia katika viwanda vya teknolojia ya hali ya juu, vikiwemo vya magari.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




