Pakistan yapokea shehena ya kwanza ya msaada wa China kwa waathirika wa mafuriko (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 30, 2025
Pakistan yapokea shehena ya kwanza ya msaada wa China kwa waathirika wa mafuriko
Picha hii ikionesha Vitu vya msaada kwa waathirika wa mafuriko vilivyotolewa na serikali ya China vilivyowasilishwa katika wilaya ya Rawalpindi, mashariki mwa Pakistan, Septemba 28, 2025. (Xinhua/Ahmad Kamal)

ISLAMABAD – Mamlaka ya kudhibiti maafa ya Pakistan imesema katika taarifa yake ya jana Jumatatu kuwa, Shehena ya kwanza ya vitu vya msaada wa dharura kwa waathirika wa mafuriko vilivyotolewa na serikali ya China imewasilishwa Pakistan juzi Jumapili, ambapo ndege mbili za China zilizobeba mahema 300 na mablanketi 9,000 zilitua katika wilaya ya Rawalpindi mashariki mwa Pakistan, ikionyesha uungaji mkono wa kudumu wa China kwa Pakistan katika nyakati za shida.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada huo, Waziri wa Pakistan anayeshughulika na Masuala ya Kashmir na Gilgit-Baltistan na SAFRON, Amir Muqam ametoa shukrani za dhati kwa serikali na watu wa China kwa uungaji wao mkono wa haraka, akisema kwamba msaada huo utaleta unafuu unaohitajika sana kwa maelfu ya familia zilizoathiriwa na mafuriko.

"Tangu mwezi Juni mwaka huu, mvua kubwa imesababisha mafuriko na maafa mengine kote Pakistan, ikisababisha mamia ya majeruhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu, nyumba na mazao ya kilimo," amesema, akiongeza kuwa msaada huo kutoka China utatoa mchango mkubwa katika jitihada za kuokoa na kutoa msaada.

Balozi wa China nchini Pakistan Jiang Zaidong amesema kuwa msaada huo unaotolewa na China umeonesha hali ya kufuata moyo wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, kusimama pamoja katika nyakati za dhiki na faraja.

Amesema kuwa chini ya uongozi wa serikali ya Pakistan na kwa uungaji mkono wa sekta zote za jamii, watu katika maeneo yaliyokumbwa na maafa wataweza kuzishinda athari za mafuriko na kujenga upya makazi yao. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha