

Lugha Nyingine
Jeshi la Sudan latangaza "mafanikio makubwa ya operesheni" katika Eneo la Kordofan
KHARTOUM – Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) vilitangaza juzi Jumamosi kuwa vimepata ushindi mkubwa katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) katika Eneo la Kordofan, magharibi mwa Sudan.
"Jimbo la Kordofan Kaskazini linashuhudia mafanikio makubwa ya operesheni, ikiwemo kuua mamia ya wanamgambo, kukamata magari zaidi ya 100 ya kivita, na kukombolea maeneo kadhaa," ofisi ya msemaji wa SAF imesema katika taarifa.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa Abdel Fattah Al-Burhan, Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Utawala la Sudan TSC na kamanda wa SAF, ametembelea mji wa kimkakati wa Bara, ambao jeshi hilo liliuteka tena Septemba 11.
Mapigano makali yamekuwa yakiendelea tangu Ijumaa usiku wiki iliyopita kati ya SAF na RSF kwenye viunga vya magharibi vya El Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini.
Wenye habari kwenye uwanja wa vita wanasema SAF, ikiungwa mkono na vikosi vya washirika, imeuteka tena mji wa Um Sumaima, magharibi mwa El Obeid karibu na mpaka wa Kordofan Kaskazini na Magharibi. Eneo hilo limekuwa likibadilisha ushikiliwaji mara kadhaa kati ya pande hizo mbili.
Vikosi Maalumu vya SAF vimesema katika taarifa kwamba vimewafukuza wanajeshi wa RSF kutoka Um Sumaima, vikiwasukuma umbali wa kilomita takriban 50 magharibi mwa El Obeid kuelekea viunga vya Al-Khuwei, mji ulioko Kordofan Magharibi.
Kwa upande wake, RSF imesema imezuia shambulizi lililoongozwa na SAF kwenye nyanja nyingi za mstari mbele magharibi mwa El Obeid.
"Tumeingiza hasara kubwa katika askari na vifaa kwa vikosi vinavyoshambulia. Vikosi vyetu vinabaki katika nafasi zao na vimedhamiria kusonga mbele kuelekea maeneo mapya ya mstari wa mbele katika maandalizi ya kuendelea kusonga mbele kuelekea ngome za adui." RSF imesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma