

Lugha Nyingine
Mazungumzo Duniani juu ya Usimamizi wa AI yazinduliwa katika Umoja wa Mataifa
UMOJA WA MATAIFA – Mazungumzo Duniani juu ya Usimamizi wa Akili Mnemba (AI) yamezinduliwa rasmi jana Alhamisi kwenye Umoja wa Mataifa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres akizungumza katika Mkutano usio rasmi wa Ngazi ya Juu wa Wadau Mbalimbali wa kuzindua mazungumzo hayo amesema "Swali si tena kama AI itaifanyia mageuzi dunia yetu - tayari inafanya hivyo.”
"Swali ni kama tutasimamia mageuzi haya kwa pamoja -- au kuyaacha yatusimamie," amesema.
Akikumbushia kuwa mwaka mmoja uliopita, Mkataba wa Kidijitali Duniani, mkataba wa kwanza wa kimataifa kuhusu usimamizi wa AI, ulipitishwa katika Umoja wa Mataifa, Guterres amesema misingi ya mfumo ikolojia wa AI duniani imewekwa leo (jana Alhamisi) ambayo inaweza kwenda sambamba na teknolojia inayokwenda kwa kasi zaidi katika historia ya binadamu.
Mfumo huo unategemea nguzo tatu za msingi -- sera, sayansi na uwezo, amesema, na kuongeza "Huo ni ushirikiano wa pande nyingi katika ubora wake -- unyumbufu, jumuishi, na unaotegemea uwajibikaji wa pamoja."
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa malengo ya Mazungumzo Duniani yako wazi: kusaidia kujenga mifumo ya AI iliyo salama, yenye ulinzi na inayoaminika; kuhimiza ushirikiano kati ya mifumo ya usimamizi; na kuhamasisha uvumbuzi wazi unaopatikana kwa wote.
"Umoja wa Mataifa unatoa jukwaa la kipekee kwa wote duniani kwa ushirikiano kama huo duniani, na kwa mara ya kwanza, kila nchi itakuwa na nafasi katika sekta ya AI," amesema.
Kwa mujibu wa Guterres, Mazungumzo Duniani yatatilia mkazo athari za AI katika mambo yake yote -- kijamii na kiuchumi, kimaadili na kiufundi, kitamaduni na lugha, na yatakamilishana na juhudi zilizopo duniani kote, zikiwemo za OECD, G7 na mashirika ya kikanda, na kutoa maskani jumuishi, tulivu kwa juhudi za kuratibu usimamizi wa AI.
Mkutano huo wa ngazi ya juu, uliofanyika pembezoni mwa Wiki ya Ngazi ya Juu inayoendelea ya mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, umeleta pamoja nchi wanachama, waangalizi, mashirika maalumu ya Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali kuzindua Mazungumzo Duniani Juu ya Usimamizi wa AI na kutilia maanani vipengele muhimu vya usimamizi jumuishi na unaowajibika wa AI.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma