IMF yapunguza makadirio ya ukuaji wa Afrika Kusini huku kukiwa na wasiwasi wa ushuru

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 24, 2025
IMF yapunguza makadirio ya ukuaji wa Afrika Kusini huku kukiwa na wasiwasi wa ushuru
Watu wakiwa kwenye maonyesho ya World Travel Market (WTM) Africa 2025 mjini Cape Town, Afrika Kusini, Aprili 11, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

JOHANNESBURG - Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limepunguza makadirio yake ya ukuaji uchumi wa Afrika Kusini mwaka 2025 kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 1, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mtazamo wa Uchumi Duniani iliyotolewa Jumanne wiki hii.

Ikirejelea "viwango vya ushuru kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana katika miaka mia moja iliyopita na mazingira yasiyotabirika sana," ripoti hiyo pia imepunguza makadirio ya ukuaji wa Afrika Kusini mwaka 2026 kutoka asilimia 1.5 ya awali hadi asilimia 1.3.

Dawie Roodt, mchumi mkuu wa Efficient Group, kampuni ya huduma za mambo ya kifedha yenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa marekebisho hayo kushuka chini hayakuja kwa kushangaza, kutokana na uwezekano wa madhara ya ushuru wa kibiashara na kukosekana utulivu duniani.

Huku sekta za kilimo na magari za Afrika Kusini zikisafirisha kuuza nje bidhaa zenye thamani ya mabilioni kwenda Marekani kila mwaka, ushuru huo unatarajiwa kuharibu sekta hizo iwapo hautabadilishwa.

Ushuru wa biashara utakuwa miongoni mwa masuala muhimu yatakayojadiliwa kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa Kundi la 20 (G20) mjini Washington wiki hii, Roodt amesema.

"Ushuru litakuwa suala kuu," amesema, akiongeza kuwa; "Ushuru na athari zake na kile ambacho nchi zinapaswa kufanya kupunguza athari zake vitajadiliwa. Mfumo wa kifedha, mfumo wa malipo, na mfumo wa akiba duniani pia itajadiliwa."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha