

Lugha Nyingine
China na Iran zabadilishana maoni kwa kina juu ya maendeleo mapya ya suala la nyuklia la Iran
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo na mwenzake wa Iran Seyed Abbas Araghchi mjini Beijing, China jana Jumatano, huku pande hizo mbili zikibadilishana maoni kwa kina juu ya maendeleo mapya ya suala la nyuklia la Iran.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amesema urafiki kati ya China na Iran umekabiliana na changamoto za kimataifa, na kwamba kuendeleza uhusiano kati ya China na Iran ni chaguo la kimkakati la pamoja kwa pande zote mbili.
Amesema, katika miaka ya hivi karibuni, China na Iran zimezidisha hali ya kuaminiana kisiasa kupitia kuungana mkono, kukaza muunganisho kati ya maslahi yao kupitia ushirikiano wa kivitendo, na kuungana na kushirikiana katika mapambano dhidi ya ukandamizaji wa upande mmoja.
"Dunia ya leo imejaa misukosuko. Marekani kutumia vibaya mbinu za ushuru, imepoteza uungwaji mkono wa watu na kuifanya nchi yenyewe ijitenge na jumuiya ya kimataifa. Jumuiya ya kimataifa inahitaji mshikamano zaidi kuliko wakati mwingine wowote ili kushikilia ushirikiano wa pande nyingi na kulinda kanuni za msingi za kulinda uhusiano wa kimataifa," Wang amesema.
Amesema China inapenda kushirikiana na Iran ili kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa kati ya viongozi wa nchi hizo mbili, na kuongeza kila mara uratibu na ushirikiano katika kuzidisha ushirikiano wa kirafiki katika nyanja mbalimbali za masuala ya kimataifa na kikanda.
Amesema, China pia inapenda kushirikiana na Iran kuhimiza ushawishi mkubwa zaidi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, mfumo wa BRICS na mifumo mingine ya pande nyingi, na kufanya juhudi zaidi kulinda maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili, vilevile juhudi za kuhimiza amani na utulivu wa kikanda na wa dunia.
Kwa upande wake Araghchi amesema kuwa Iran inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano wake na China, inafuata kanuni ya kuwepo kwa China moja, na inaiunga mkono China katika kulinda maslahi yake makuu.
Amesema, Iran itaendelea kuungana mkono kithabiti, kupinga msimamo wa upande mmoja na ubabe, na kulinda ushirikiano wa pande nyingi.
Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Wang amesisitiza kuwa, China siku zote imekuwa ikijizatiti katika suluhu ya kisiasa na kidiplomasia ya suala la nyuklia la Iran, na inapinga matumizi mabaya ya nguvu na vikwazo haramu vya upande mmoja.
Naye Araghchi amepongeza mchango muhimu wa China katika kuhimiza utatuzi wa kisiasa na kidiplomasia wa suala hilo la nyuklia la Iran, na kuelezea nia yao ya kudumisha mawasiliano na uratibu wa karibu na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma