UN yadhimisha Siku ya Lugha ya Kichina kwa shughuli changamani za kitamaduni

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 17, 2025
UN yadhimisha Siku ya Lugha ya Kichina kwa shughuli changamani za kitamaduni
Zach Danz, mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisoma sehemu ya Kitabu cha Mabadiliko kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya 16 ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kichina kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Aprili 15, 2025. (Xinhua/Li Rui)

UMOJA WA MATAIFA - Umoja wa Mataifa (UN) umeadhimisha Siku yake ya 16 ya Lugha ya Kichina Jumanne wiki hii kwenye makao makuu yake mjini New York, ikitoa shughuli za kitamaduni ambazo zilichanganya mashairi na muziki wa Kichina ambapo hafla hiyo ya mwaka huu, yenye kaulimbiu ya "China ya Kishairi: Kibwagizo na Mahaba," imehusisha usomaji wa mashairi ya Kichina, burudani ya muziki, na maonyesho ya maandishi ya Kichina huku wanadiplomasia, wafanyakazi wa UN na wageni wa kimataifa zaidi ya 400 wakihudhuria.

Shughuli hiyo ilionyesha utumbuizaji wa waimbaji wa Umoja wa Mataifa, ambao, wakiwa wamevalia mavazi ya kijadi, waliimba wimbo mashuhuri wa Kichina "Jasmine." Aidha, wafanyakazi na wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa walisoma nukuu kutoka vitabu bora vya Kichina, zikiwemo za Kitabu cha Mashairi na Kitabu cha Mabadiliko, vilevile shairi lilolotungwa na kampuni ya AI ya China, DeepSeek, likionyesha uzuri wa mashairi ya lugha ya Kichina.

Zach Danz, mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mmoja wa wasomaji, alianza kujifunza Lugha ya Kichina muongo mmoja uliopita alipokuwa akisoma sanaa za jukwaani katika chuo kikuu cha Shanghai. Ingawa amekubali changamoto za kuifahamu vema lugha hiyo, Danz ameelezea namna anaona ni bora kufuatilia utamaduni wa Kichina.

Kwenye hafla ya ufunguzi, Fu Cong, mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, amesema kuwa ushairi umejikita sana katika nafsi ya watu wa China. Amebainisha kuwa ushairi bora wa kijadi wa Kichina, ambao ulianza zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, uliashiria mwanzo wa utamaduni tajiri wa jadi.

Fu amesisitiza kuwa "Wachina wanazidi kujiamini zaidi kwenda kwenye jukwaa la dunia, wakiwa ni daraja linalovuka tamaduni, kujenga maelewano na kusaidia kujenga mapatano."

Siku za Lugha za Umoja wa Mataifa, zilizoanzishwa mwaka 2010, zinahimiza hali ya uwepo wa lugha nyingi na uanuwai wa kitamaduni, na kuhakikisha matumizi sawa ya lugha sita rasmi za Umoja wa Mataifa: Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania.

Siku ya Lugha ya Kichina huadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Aprili, karibu na kipindi cha Guyu (Mvua ya Mtama), kipindi cha sita kati ya 24 katika kalenda ya kilimo ya China. Tarehe hii inamkumbuka Cangjie, mtu mashuhuri anayeaminika kuvumbua herufi za Kichina.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha