

Lugha Nyingine
China yazindua njia ya kwanza ya malori makubwa yanayotumia nishati ya hidrojeni
BEIJING – Shirika la Mafuta la China, Sinopec, limetengaza uzinduzi rasmi wa njia ya kwanza ya kuvuka mikoa kwa malori ya kubeba mizigo yanayotumia nishati ya hidrojeni, ikiashiria hatua muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nishati ya hidrojeni katika mikoa ya magharibi ya China.
Njia hiyo, ambayo sasa inafanya kazi kwa huduma za kawaida za uchukuzi kupitia malori yenye kutumia nishati ya hidrojeni, ina urefu wa kilomita 1,150 kutoka Mji wa Chongqing, kusini-magharibi mwa China hadi Bandari ya Qinzhou katika Mkoa wa Guangxi ikipitia Mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China.
Njia hiyo ina vituo vinne vya kujaza hidrojeni, vyote vikiwa vimejengwa na Sinopec, ili kuhakikisha mtandao wa uhakika wa usambazaji hidrojeni njiani.
Mikoa hiyo ina rasilimali nyingi za hidrojeni, na uwepo wa teknolojia za uzalishaji wa hidrojeni kama vile za utenganishaji wa hidrojeni kutoka kwenye maji na mtengano wa amonia. Ikiwa na uzalishaji wa mwaka wa ziada wa hidrojeni inayozidi tani 400,000 – mikoa hiyo kwa pamoja inaweza kukidhi mahitaji ya mafuta ya magari ya uchukuzi 360,000 yanayotumia hidrojeni.
Mbali na usafirishaji, ushoroba huo hutumika kama muunganisho wa viwanda. Unakadiriwa kushughulikia mizigo 220,000 ya shehena kwa mwaka kwenda na kurudi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma