

Lugha Nyingine
Safari za ndege za moja kwa moja kati ya Beijing na Tel Aviv zarejeshwa baada ya kusimama kwa miezi 18 (5)
![]() |
Abiria wakishuka kutoka Ndege ya Shirika la Ndege la Hainan, ndege ya kwanza ya abiria kurejesha safari ya moja kwa moja kati ya Beijing na Tel Aviv, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben-Gurion karibu na Tel Aviv, Israel, tarehe 10 Aprili 2025. (Xinhua/Chen Junqing) |
JERUSALEM - Safari za ndege za moja kwa moja kati ya miji ya Beijing, China na Tel Aviv, Israel zimerejeshwa jana Alhamisi, huku ndege ya Shirika la Ndege la Hainan ikitua kwa mafanikio kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben-Gurion karibu na Tel Aviv mapema asubuhi ya siku hiyo, ikiashiria mwisho wa kusimama kwa huduma hiyo kwa miezi 18.
Kwa mujibu wa Yu Chaojie, Mkuu wa Shirika la Ndege la Hainan, njia hiyo iliyorejeshwa kati ya Beijing na Tel Aviv itafanya safari mbili za ndege kwenda na kurudi kwa wiki, Jumatatu na Alhamisi, zikiwa na muda wa safari wa saa takriban tisa.
Shirika hilo la ndege la China kwa sasa pia linaendesha njia ya usafiri wa anga inayounganisha Tel Aviv na Shenzhen, mji mkubwa wa kisasa kusini mashariki mwa China.
Kwenye hafla ya kurejeshwa kwa safari za ndege hiyo iliyofanyika Tel Aviv, Chen Arieli, naibu meya wa Tel Aviv, ameelezea shukrani zake kwa kurejea kwa safari hizo za ndege, akisisitiza mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya China na Israel.
Njia hiyo ya anga kati ya Beijing na Tel Aviv ilizinduliwa kwa mara ya kwanza Aprili 2016, ikilifanya shirika hilo la ndege kuwa la kwanza nchini China kufanya safari za moja kwa moja hadi Israel. Kutokana na kuzuka kwa mgogoro kati ya Israel na Hamas mwezi Oktoba 2023, safari za ndege za moja kwa moja kutoka Beijing na Shanghai hadi Israel zilisitishwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma