Wito wa "kamwe tena" kwa mauaji ya kimbari wasisitizwa tena wakati ubalozi wa Rwanda mjini Beijing ukiandaa Kwibuka 31 (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 09, 2025
Wito wa
He Degang, Mwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China akitoa hotuba kwenye shughuli hiyo. (Picha kwa hisani: Ubalozi wa Rwanda nchini China)

BEIJING - Wakati ubalozi wa Rwanda mjini Beijing, China Jumatatu, Aprili 7 ukiungana na jumuiya ya kimataifa kuanza siku 100 za kuadhimisha miaka 31 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Kwibuka 31, maafisa na mabalozi wa ujumbe wa kidiplomasia nchini China wamesisitiza wito wa "kamwe tena" kwa mauaji ya kimbari kutokea mahali popote duniani, wakihimiza tafakari ya kina na kujifunza somo kutoka kwenye historia kwa ajili ya mustakabali wa baadaye wenye amani na wa pamoja wa binadamu.

Akitoa hotuba kuu ya shughuli hiyo, Balozi wa Rwanda nchini China James Kimonyo amerejelea mauaji hayo ya kimbari, akisema kuwa Aprili 7, 1994, mauaji hayo yalianza kote nchini Rwanda ambapo Watutsi milioni moja wasio na hatia waliuawa kwa siku 100 (miezi 3). "Mauaji haya ya kutisha yalitokea kwa kasi ya kutisha! Inakadiriwa kuwa watu 10,000 walichinjwa kila siku" amesema.

Wakati dunia inakumbuka na kuomboleza waathiriwa wa mauaji ya kimbari ya Watutsi wa Rwanda, Balozi huyo amesema, inaonekana kwamba dunia haijatafakari na kujifunza kutoka kwenye historia kwani kuna matukio kama haya ambayo yanaongezeka polepole kuelekea mauaji mapya ya kimbari.

"Tunapokumbuka, ngoja niulize swali rahisi. Je, tumejifunza chochote kutokana na kushindwa huko kwa binadamu? Ni nini kilitokea kwa ahadi ya "kamwe tena" ambayo dunia ilitoa baada ya mauaji ya Holocaust? Je, ilishindwa au ilipuuza? Ninaweza kusema bila woga au upendeleo kwamba inaonekana hatujajifunza masomo ya kutosha” amehoji na kusisitiza.

Akitoa hotuba yake, He Degang, Mwakilishi wa Serikali ya China amesema kuwa, maafa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 si tu yalileta mateso kwa watu wa Rwanda, bali pia yameacha somo chungu kwa jumuiya ya kimataifa.

Hata hivyo, amesema, chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame, serikali na watu wa Rwanda wamejiondoa kwenye giza hilo la kihistoria, wamepata maridhiano ya kitaifa, wamedumisha utulivu wa kitaifa na maelewano ya kijamii, na kufikia ukuaji wa haraka wa uchumi.

Huku akisema kuwa, mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 80 tangu kupatikana ushindi wa Vita vya Watu wa China dhidi ya Uvamizi wa Japan na Vita vya Dunia dhidi ya Ufashisti, pamoja na maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, He amesema, mwaka huu maalum unaonyesha umuhimu wa kuweka mtazamo sahihi wa kihistoria.

Amesema hali ya kimataifa inayobadilika na yenye misukosuko inaonyesha zaidi umuhimu wa pendekezo la Rais Xi Jinping wa China la kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu na mapendekezo ya kimataifa aliyoyatoa ambayo ni; Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia, na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia.

Balozi Martin Mbana, Mkuu wa Ujumbe wa Wanadiplomasia nchini China, amesema kuwa maadhimisho ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, yanakumbusha nchi zote uzito wa tishio hili na wajibu wa kupinga tabia ya kujiangamiza ya vitendo hivi vyote vya uhalifu.

"Miaka 31 baada ya mauaji ya kimbari, watu wa Rwanda wametufundisha somo muhimu kwa kutuonyesha namna ya kuondokana na chuki na mateso na kuchagua umoja na upatanisho kwa toba na msamaha" amesema.

Akitoa hotuba yake katika shughuli hiyo, Kaimu Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini China, Li Changhui, amesema watu wamekusanyika katika siku hiyo ya kumbukumbu ya Kwibuka 31, kukumbuka ukatishaji maisha ya watu wasio na hatia uliofanywa kikatili, kusimama kwa mshikamano na walionusurika, na kamwe kutokurudia tena.

Kwa mujibu wa Kimonyo, Kwibuka ya mwaka huu yenye kaulimbiu ya "kumbuka-unganisha-ukarabati" itatiliwa maanani na kuadhimishwa duniani kote kwa siku 100 kuanzia Aprili 7, ikijumuisha maonyesho, mihadhara ya umma, ushuhuda kutoka kwa waathirika wa mauaji ya kimbari na shughuli nyingine nyingi, huku bendera ya Rwanda ikipeperushwa nusu mlingoti katika siku saba za kwanza. Nchini China, shughuli mbalimbali zitafanyika katika maeneo mbalimbali katika siku hizo 100.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha