Maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Trump yafanyika Marekani na Ulaya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 07, 2025
Maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Trump yafanyika Marekani na Ulaya
Picha iliyopigwa Agosti 4, 2022 ikionyesha Ikulu ya White House na ishara ya kusimama mjini Washington, D.C., Marekani. (Xinhua/Liu Jie)

BEIJING - Mamia ya maelfu ya waandamanaji wamekusanyika katika miji kadhaa katika sehemu mbalimbali nchini Marekani na Ulaya juzi Jumamosi kupinga sera tata za utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, ikiwemo uwekaji wa kile kinachoitwa "ushuru wa Reciprocal," ufungaji wa mashirika ya serikali kuu ya Marekani na kufukuzwa kwa wahamiaji.

Nchini Marekani, watu karibu 600,000 walijiunga na maandamano zaidi ya 1,400 katika majimbo yote 50 ya nchi hiyo chini ya kaulimbiu ya "Toa Mikono," kwa mujibu wa waandaaji.

Wakiwa wameratibiwa na muungano wa vikundi zaidi ya 150, ikijumuisha mashirika ya haki za kiraia, jumuiya za wafanyakazi na jumuiya za wanajeshi wastaafu, waandamanaji hao walikusanyika katika miji mikuu ya majimbo, majengo ya serikali kuu, ofisi za mabunge, makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii, kumbi za miji na bustani za umma.

"Harakati hiyo ya amani inaendeshwa na watu wa kawaida -- wauguzi, walimu, wanafunzi, wazazi -- ambao wanainuka kulinda kile ambacho ni muhimu zaidi. Tumeungana, hatukati tamaa, na ndiyo tunaanza," amesema Rahna Epting, mkurugenzi mtendaji wa kundi la wanaharakati la MoveOn.

Tuko hapa kupigania roho ya Marekani," Angela C, mwandamanaji mjini Los Angeles, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Baadhi ya maofisa waliochaguliwa wamejiunga na kampeni hiyo pia. Meya wa Boston Michelle Wu amesema hataki watoto wake na watu wengine waishi katika dunia ambapo vitisho na kuogopesha ni njia za serikali na maadili kama vile uanuwai na amani viko chini ya mashambulizi.

Katika kujibu maandamano hayo, Ikulu ya White House imesema kwenye taarifa yake kwamba "Rais Trump hatazuiwa kutekeleza ahadi alizotoa za kuifanya serikali yetu kuu kuwa fanisi zaidi na kuwajibika zaidi kwa walipakodi wa Wamarekani wachapakazi kote nchini ambao walimchagua tena kwa kura nyingi," kwa mujibu wa jarida la USA Today.

Maandamano pia yamefanyika katika miji ya Ulaya kama vile Berlin, Frankfurt, Paris, London na Lisbon. Mjini Berlin, mamia ya watu walikusanyika nje ya duka la kuuza magari la Tesla kupinga mmiliki wa Tesla, Elon Musk, ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Trump.

Jijini London, waandamanaji walikusanyika katika Eneo la Wazi la Trafalgar, wakiwa na mabango yenye maandishi “Mmarekani Mjivuni Anaaibika” (Proud American Ashamed) na wakitamka kaulimbiu ya "Toa Mkono kwa Canada" na "Toa Mkono kwa Greenland."

Maandamano hayo ya barani Ulaya yamekuja siku chache baada ya Trump kuweka ushuru wa "Raciprocal" wa asilimia 20 kwa bidhaa za kuagizwa kutoka EU, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio akihudhuria mkutano wake wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO mjini Brussels mapema wiki hii -- unaotazamwa na wengi kama juhudi za kudhibiti mvutano kati ya pande hizo mbili za Atlantiki kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa NATO mwezi Juni.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha