China na Tanzania zawaomboleza wahanga wa China katika ujenzi wa reli ya TAZARA

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2025
China na Tanzania zawaomboleza wahanga wa China katika ujenzi wa reli ya TAZARA
Watu wakiweka maua kwenye jiwe la kaburi la mtaalamu wa China kwenye makaburi ya Gongo la Mboto nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 2, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM - China na Tanzania zimefanya shughuli ya kuweka mashada ya maua kwenye makaburi ya Gongo la Mboto nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana Jumatano, zikiwaomboleza wataalam 70 wa China waliojitoa mhanga maisha yao wakati wakijenga Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) miaka ya 1970.

Shughuli hiyo ya kumbukumbu imefanyika wakati wa Siku ya Qingming, ambapo Wachina huomboleza marehemu na kukumbuka mababu. Wawakilishi kutoka Ubalozi wa China nchini Tanzania, serikali ya Tanzania, sekta mbalimbali za kijamii, na jumuiya ya Wachina walishiriki kwenye shughuli hiyo.

Chini ya anga yenye kumetameta, washiriki waliovalia suti nyeusi walitafakari kidhati juu ya kujitoa mhanga kwa wataalamu hao wa China na mchango wao wa muda mrefu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania na Zambia.

"Serikali za Tanzania na Zambia zitakumbuka milele kujitoa mhanga kwa watu wa China wakati wa ujenzi wa njia hii ya reli," amesema Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania David Kihenzile, akisema kuwa mradi huo ulijaa changamoto na hatari, zikihitaji ushujaa na werevu kutoka kwa wafanyakazi wa China na wenyeji wa Tanzania na Zambia.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Bruno Ching’andu amepongeza moyo wa kujitolea wa wataalamu hao wa China, akisema kujitolea kwao kulifanikisha ujenzi wa reli hiyo.

“Roho zao zinaonyeshwa katika kila treni inayopita. Roho zao zinaonyeshwa katika kila tani ya mizigo inayosogezwa," amesema Ching'andu.

Kaimu Balozi wa ubalozi wa China nchini Tanzania Wang Yong amewaelezea wataalam hao kuwa ni mashujaa ambao urithi wao unaendelea kuonyesha urafiki wa China-Tanzania na China na Afrika.

"Wataishi milele katika mioyo ya watu wa China na Tanzania, kama vile reli ya TAZARA inavyosimama kama ushuhuda wa juhudi zao," amesema.

Reli ya TAZARA, inayojulikana kwa jina la "Reli ya Uhuru", ilijengwa kama mradi wa kuhitaji kutumika haraka kati ya 1970 na 1975 kupitia mkopo usio na riba kutoka China. Uendeshaji kibiashara ulianza Julai 1976, ikichukua urefu wa kilomita 1,860 kutoka Dar es Salaam nchini Tanzania hadi New Kapiri Mposhi nchini Zambia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha