Bunge la Afrika Kusini lapitisha bajeti ya 2025 licha ya kupinga ongezeko la VAT

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2025
Bunge la Afrika Kusini lapitisha bajeti ya 2025 licha ya kupinga ongezeko la VAT
Mwenyekiti wa Bunge la Afrika Kusini Cedric Frolick (katikati) akitangaza matokeo ya kura juu ya Bajeti ya 2025 bungeni mjini Cape Town, Afrika Kusini, Aprili 2, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

CAPE TOWN - Bunge la Afrika Kusini limepitisha Bajeti ya 2025 jana Jumatano iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Enoch Godongwana, licha ya kuna upinzani mkubwa juu ya ongezeko tata la kodi ya kuongeza thamani (VAT) ambapo mswada wa sheria ya bajeti hiyo umeidhinishwa kwa tofauti ndogo, huku wabunge 194 wakipiga kura ya ndiyo na 182 ya hapana, wakati huohuo hakukuwa na mbunge aliyejizuia kupiga kura.

Ikiwa awali ilipangwa kuwasilishwa mwezi Februari, bajeti hiyo ilicheleweshwa kwa sababu ya maoni ya tofauti ya ndani juu ya mapendekezo ya kuongeza VAT. Machi 12, Godongwana aliwasilisha mapitio ya bajeti hiyo bungeni, akielezea ongezeko la VAT kwa awamu ili kukabiliana na upungufu wa fedha wa serikali. Chini ya mpango huo, VAT itapanda kwa asilimia 0.5 mwaka 2025/26 na asilimia nyingine 0.5 mwaka unaofuata, ikifikisha kiwango hicho katika asilimia 16 ifikapo mwaka wa fedha 2026/27.

Kwenye hotuba yake ya bajeti, Godongwana ametetea ongezeko hilo la kodi linalohitajika ili kukidhi huduma za umma huku kukiwa na shinikizo la kibajeti katika sekta muhimu kama vile afya, elimu, usafiri na usalama.

Hata hivyo, ongezeko hilo limezua upingaji mkali wa kisiasa. Chama cha Democratic Alliance (DA), chama cha pili kwa ukubwa katika muungano unaotawala, kimeikataa bajeti hiyo, kikirejelea wasiwasi wa ongezeko hilo la kodi na vipaumbele vya matumizi ya serikali. Awali Godongwana alisema kuwa chama cha DA kilionyesha uungaji mkono wake kwa masharti, ikiwa tu serikali itaondoa Sheria ya Kutwaa Ardhi.

Baada ya wiki kadhaa za majadiliano ya kisiasa na mijadala mikali, chama tawala cha African National Congress kilipata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa washirika wa vyama vidogo vinavyounda muungano unaotawala serikali na makundi mengine ya kisiasa ili kupitisha bajeti hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha