Trump atia saini amri tendaji juu ya "ushuru wa kutozana sawa" huku kukiwa na upingaji mkubwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2025
Trump atia saini amri tendaji juu ya
Rais Donald Trump wa Marekani akionyesha amri tendaji juu ya "ushuru wa kutozana sawa" katika Rose Garden ya Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Aprili 2, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Huku kukiwa na upingaji mkubwa, Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri tendaji jana Jumatano juu ya kile kinachoitwa "ushuru wa kutozana sawa," akiweka "ushuru wa chini" wa asilimia 10 na viwango vya juu kwa baadhi ya wenzi wake wa kibiashara ambapo amri hiyo tendaji inasema kuwa bidhaa zote zinazoingia Marekani zitatozwa asilimia 10 ya ushuru wa ziada, isipokuwa itakapoelezekezwa vinginevyo, na itaanza kutekelezwa Aprili 5.

Trump ataweka "ushuru wa juu zaidi wa kutozana sawa" kwa nchi na maeneo ambayo Marekani "ina nakisi kubwa zaidi ya biashara," kwa mujibu wa nyaraka ya Ikulu ya White House. Inaeleza ushuru huo utaanza kutozwa Aprili 9.

"Baadhi ya bidhaa hazitaguswa na ushuru huo wa kutozana sawa, zikiwemo za chuma na aluminiamu, vilevile magari na vipuri vya magari ambazo tayari zimetozwa ushuru wa Kifungu cha 232, shaba, dawa, semikondakta na mbao," Ikulu ya White House imesema.

Kwa Canada na Mexico, bidhaa zinazotajwa kwenye Makubaliano ya Marekani-Mexico-Canada (USMCA) zitaendelea kutozwa ushuru wa asilimia 0, bidhaa zisizotajwa kwenye USMCA zitastozwa ushuru wa asilimia 25, na nishati na potashi zisizotajwa kwenye USMCA zitatozwa ushuru wa asilimia 10, kwa mujibu wa Ikulu ya White House.

Kwenye hotuba yake katika Rose Garden ya White House, Trump aliwasilisha chati kuhusu "ushuru wa kutozana sawa." Chati hiyo inaonyesha kuwa nchi na maeneo tofauti yanakabiliwa na viwango tofauti vya ushuru.

Kwa mfano, China itakabiliwa na ushuru wa asilimia 34, Umoja wa Ulaya asilimia 20, Vietnam asilimia 46, Japan asilimia 24, India asilimia 26, Korea Kusini asilimia 25, Thailand asilimia 36, Uswisi asilimia 31, Indonesia asilimia 32, Malaysia asilimia 24 na Cambodia asilimia 49.

Trump amedai kuwa wenzi wake wengine wa kibiashara huweka "vizuizi visivyo vya kifedha" kwa Marekani. Chati hiyo inaonyesha viwango tofauti vya ushuru "unaotozwa" na nchi au maeneo mbalimbali dhidi ya Marekani, ikiwa ni pamoja na "uhodhi wa thamani ya sarafu" na "vizuizi vya biashara."

"Hakuna msingi wa viwango vinavyodaiwa kuwa ushuru wa usawa uliowekwa na nchi nyingine. Hii ni uongo tupu," Gary Clyde Hufbauer, mtafiti mwandamizi asiye wa kudumu katika Taasisi ya Peterson kwa Uchumi wa Kimataifa, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Licha ya madai ya Trump kwamba ushuru wa juu utasaidia kuleta mapato kwa serikali na kufufua viwanda vya Marekani, wanauchumi wameonya kuwa hatua kama hizo zitaongeza bei kwa watumiaji na biashara za Marekani, kuvuruga biashara ya kimataifa, na kuharibu uchumi wa dunia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha