Mkuu wa EU aapa kulipiza vikali kama ushuru wa Marekani utaongezeka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 02, 2025
Mkuu wa EU aapa kulipiza vikali kama ushuru wa Marekani utaongezeka
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen akihutubia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa, Aprili 1, 2025. (Umoja wa Ulaya/kupitia Xinhua)

BRUSSELS - Umoja wa Ulaya (EU) umeweka mpango thabiti wa kulipiza dhidi ya ushuru wa Marekani na itachukua hatua kama inahitajika, Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Jumanne alipokuwa akihutubia Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa jana Jumanne.

EU "haikuanzisha mzozo huu" lakini iko tayari kulinda watu wake na ustawi wake, von der Leyen amesema.

"Hatutaki kulipiza. Lakini kama ni lazima, tuna mpango mkubwa wa kulipiza, na tutautumia," amesema.

Kauli yake inafuatia uamuzi wa utawala wa Trump wa kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa chuma, aluminiamu, magari na vipuri vya magari. Von der Leyen ameonya kuwa ushuru zaidi unaweza kulenga watengenezaji wa semikondakta, dawa na mbao, huku raundi mpya ya ushuru huenda kutangazwa mapema leo Jumatano.

Amekosoa hatua hiyo ya Marekani kwa kuielezea kuwa ni isiyo na tija, akisema itadhuru viwanda vya Ulaya na watumiaji wa Marekani.

"Ushuru ni kodi ambayo italipwa na watu," von der Leyen amesema, akiongeza kuwa watumiaji wa Marekani watalipa kwa ushuru huo kwenye bidhaa za chakula, matumizi ya nyumbani na dawa.

Huku akisisitiza tena nia ya EU ya kufanya mazungumzo, von der Leyen amesisitiza kwamba Brussels haitapiga magoti kwa shinikizo.

"Tuko wazi kwa mazungumzo. Tutashughulikia mazungumzo haya kutoka kwenye nafasi yenye nguvu," amesema, akibainisha "kadi" za EU katika biashara, teknolojia na ukubwa wa soko.

Von der Leyen amesema amekuwa akiwasiliana na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, na atatathmini hatua zinazofuata za Washington kabla ya kuamua mwitikio wa umoja huo.

"Lengo letu ni kutatua suala kupitia mazungumzo, lakini bila shaka, kama itahitajika, tutalinda maslahi yetu, watu wetu na kampuni zetu," ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha