

Lugha Nyingine
China na Ufaransa zakubaliana kuimarisha mazungumzo katika sekta zote na ngazi zote (2)
![]() |
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot mjini Beijing, mji mkuu wa China, Machi 27, 2025. (Xinhua/Zhang Ling) |
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Jean-Noel Barrot mjini Beijing siku ya Alhamisi, akisema kuwa China inapenda kushirikiana na Ufaransa kufuata maafikiano yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuimarisha mazungumzo katika sekta zote na ngazi zote, kuvuka tofauti na kuzidisha ushirikiano.
Amesema katika hali ya sasa ya kimataifa, China na Ufaransa zinapaswa kuchukua jukumu la nchi kubwa, kuongeza uratibu wa kimkakati, na kuunga mkono mapendekezo muhimu kuhusu mfumo wa pande nyingi yaliyotolewa na kila upande.
Akisema kuwa China inaitazama Ufaransa kama mwenzi wa kipaumbele katika kufikia maendeleo bora ya hali ya juu, Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema China inapenda kuzidisha ushirikiano na Ufaransa katika sekta za jadi, kuhimiza uwekezaji wa kila upande, na kupanua ushirikiano katika sekta zinazoibukia ili kuingiza motisha mpya katika ushirikiano wa pande mbili.
Pia ametoa wito kwa pande hizo mbili kuzidisha maelewano na urafiki ili kuimarisha msingi wa uungaji mkono wa umma.
Kwa upande wake Barrot amesifu mafanikio ya ushirikiano wa kivitendo kati ya Ufaransa na China, akisema kwamba hali ya sasa ya kimataifa ambayo hali ya kutokuwa na uhakika na kujitokeza kujihami kiuchumi inaongezeka, ikifanya uhusiano kati ya Ufaransa na China kuwa muhimu zaidi.
"Ufaransa inaichukua China kama mwenzi muhimu wa ushirikiano, inafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja, na imejitolea kuendeleza uhusiano wenye mwelekeo wa siku za baadaye na wa muda mrefu kati yake na China," amesema, akiongeza kuwa Ufaransa inaunga mkono biashara huria, inapinga kutengana kiuchumi na vita vya kibiashara.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni kuhusu uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya. Akisema kuwa ushirikiano kati ya China na Umoja wa Ulaya unashinda ushindani, na maafikiano yanapita tofauti, Wang amesema kuna mazingira ya kutosha ya kuongeza zaidi uhusiano kati ya pande hizo mbili.
Naye Barrot amesema kuwa Ufaransa inaunga mkono mazungumzo kati ya EU na China ili kutatua tofauti zao za kibiashara.
Baada ya mazungumzo hayo, China na Ufaransa zilitoa taarifa ya pamoja kuhusu mabadiliko ya Tabianchi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma