Trump atia saini amri tendaji kuanza kuvunja Wizara ya Elimu ya Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 21, 2025
Trump atia saini amri tendaji kuanza kuvunja Wizara ya Elimu ya Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump akizungumza kabla ya kutia saini amri tendaji katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Machi 20, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri tendaji jana Alhamisi kuanza rasmi mchakato wa kuvunja Wizara ya Elimu ya nchi hiyo, akisema kuwa utawala wake unarejesha masuala ya elimu katika serikali za majimbo.

Zaidi ya "mahitaji ya msingi, utawala wangu utachukua hatua zote za kisheria kuifunga wizara," Trump amesema katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Ikulu ya White House.

"Tutaifunga na kuifunga haraka iwezekanavyo," Trump amesema.

Akibainisha kuwa Wizara hiyo ya Elimu "haitufanyii mema" – akirejelea uwezo mdogo wa kusoma na hisabati miongoni mwa wanafunzi katika shule za msingi, sekondari na sekondari za juu za Marekani -- Trump amesema utawala wake unarejesha masuala ya elimu katika majimbo.

Rais huyo wa Marekani amebainisha kuwa kazi za wizara hiyo kama vile Misaada kwa Watu wenye Kipato cha Chini, Pell Grants, Title I, na rasilimali za ufadhili kwa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum, "zitahifadhiwa kikamilifu" na "zitasambazwa upya kwa mashirika na wizara nyingine mbalimbali."

"Utawala wa Trump unakinyima kizazi kijacho rasilimali hitajika, kwa ajili kulipia mabilionea punguzo la kodi. Ni usaliti kwa wanafunzi, wazazi na waelimishaji," Mwenyekiti wa Kundi la Wamarekani wenye asili ya Asia Pasifiki ya Bunge la Marekani Grace Meng na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Elimu, Mwakilishi Mark Takano wamesema katika taarifa ya pamoja.

"Huu ni uamuzi usio wa kisheria na Bunge halipaswi kuachilia mamlaka yake mbele ya amri hii," taarifa hiyo inaeleza.

Kuanzishwa na kuvunjwa kwa mashirika ya serikali kuu ya Marekani kwa kawaida kunahitaji idhini ya Bunge la Marekani kupitia sheria. Kama Trump anataka kuifunga Wizara ya Elimu, lazima iwe kupitia mchakato huo wa kisheria katika Bunge hilo. Bado haijawa wazi ni kwa namna gani ataendelea na amri hiyo tendaji.

Trump kwa muda mrefu amekuwa akiikosoa Wizara hiyo ya Elimu, akisema kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa serikali kuu katika elimu, ubora wa elimu haujakidhi matarajio, akirejelea mapungufu ya umahiri wa wanafunzi wa Marekani katika kusoma, hisabati na maeneo mengine.

Wakati huo huo, Trump amekuwa akiishutumu wizara hiyo kwa kujazwa watu wanaoshikilia itikadi za mrengo wa kushoto, hata kuielezea kuwa ni kitovu cha "wanaharakati, wakereketwa na wafuataji Umarksi," akiamini kuwa watu hao wamepanua mamlaka yao kupitia miongozo na udhibiti wa kupita kiasi.

Wizara hiyo ya Elimu awali ilianzisha upunguzaji wafanyakazi kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa ripoti za awali za vyombo vya habari vya Marekani, wizara hiyo, ambayo awali ilikuwa na wafanyakazi 4,000, ilikuwa imeshapunguza karibu nusu ya wafanyakazi wake. Trump amesema siku hiyo ya Alhamisi kwamba "upunguzaji nguvu kazi" umefanikiwa. "Tumepunguza idadi ya watendaji kwa nusu, asilimia 50," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha