Jukwaa la kimataifa la nishati, Wiki ya CERA laanza huku kukiwa na kutokuwa na uhakika kwenye soko, sera na mpito wa nishati (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 11, 2025
Jukwaa la kimataifa la nishati, Wiki ya CERA laanza huku kukiwa na kutokuwa na uhakika kwenye soko, sera na mpito wa nishati
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Saudi Aramco Amin Nasser (kwenye mimbari na kwenye skrini) akizungumza katika Wiki ya CERA mjini Houston, Texas, Marekani, Machi 10, 2025. (Picha na Zhou Yiheng/Xinhua)

HOUSTON - Viongozi wa tasnia ya nishati duniani wanakusanyika katika jiji la kusini mwa Marekani la Houston wakati ambapo Wiki ya CERA, jukwaa la kila mwaka lenye ushawishi mkubwa zaidi katika tasnia hiyo, likifunua ajenda yake jana Jumatatu huku kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika inayokabili soko la nishati na mpito kuelekea nishati safi.

"Tunakusanyika wakati wa mabadiliko makubwa, fursa na hali ya kutotabirika katika nishati na katika masuala ya kimataifa," amesema muandaaji wa jukwaa hilo, S&P Global, katika hotuba yake ya ukaribisho.

Bei ya mafuta ilishuka kwa asilimia 1 jana Jumatatu baada ya kufikia kiwango cha chini katika kipindi cha miaka mitatu chini ya dola za Kimarekani 70 kwa pipa wiki iliyopita, ikitokana na hali ya kutokuwa na uhakika juu ya ushuru wa forodha wa Marekani na wasiwasi kwamba sera za Rais Donald Trump zinavuruga mtiririko wa biashara duniani.

Likiwa na kaulimbiu ya "Kusonga Mbele: Mikakati ya Nishati kwa Dunia Tata," jukwaa hilo la 43 litashughulikia changamoto kubwa zinazohusiana na usalama wa nishati, usambazaji, na matarajio ya tabianchi, vilevile maendeleo katika masoko, miundombinu, mwelekeo wa sera, na uvumbuzi wa teknolojia -- haswa zile zinazoendeshwa na akili mnemba (AI), ajenda za jukwaa hilo zinaonesha.

Ushuru umeibuka kuwa mada kuu ya mjadala, huku wataalam wakijadili ikiwa uhusiano mpya wa "ushuru, biashara, na ushindani" utabadili soko la nishati na sera, ikiwa na uwezekano wa kuwa mbadala wa vipaumbele vya muda mrefu vya kimataifa vya "usalama, unafuu wa kumudu, na uendelevu."

"Sekta ya nishati iko katika njia panda," S&P Global imesema katika ripoti, ikirejelea mfano wa mfumuko wa bei wa juu, ukuaji duni wa uchumi, na kupanda kwa gharama za nishati miongoni mwa vichocheo vya hali ya kutokuwa na uhakika duniani, ambavyo vinazidisha mtanziko wa mpito wa nishati.

Sera ya nishati ya Marekani pia inachunguzwa vikali. Katika hotuba yake kuu siku ya Jumatatu, Waziri wa Nishati wa Marekani Chris Wright alithibitisha dhamira ya utawala wa Trump ya kuongeza uzalishaji wa mafuta ya visukuku nchini humo huku akivunja sera za tabianchi za Rais wa zamani wa Chama cha Democrat Joe Biden, ambazo amezielezea kuwa "hazifai."

Wakati wa kampeni yake ya urais 2024, Trump aliihimiza mara kwa mara tasnia ya nishati ya Marekani "chimbeni, mtoto, chimbeni." Hata hivyo, wazalishaji wa mafuta na gesi nchini humo hawana uwezekano wa kuongeza matumizi mwaka huu, kwa mujibu Lorenzo Simonelli, mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Baker Hughes, ambaye alizungumza atika jukwaa hilo siku ya Jumatatu.

Saa chache baada ya kongamano hilo kuanza, waandamanaji zaidi ya 100 waliandamana katikati mwa jiji la Houston na kukusanyika nje ya ukumbi wa Wiki ya CERA, wakilaani kampuni za mafuta na gesi na kudai haki ya tabianchi. Mashuhuda wanasema waandamanaji kadhaa walikamatwa na polisi.

Wiki ya CERA mwaka huu inakutanisha watendaji wakuu zaidi ya 450, mawaziri na maafisa wakuu 80, huku kukiwa na washiriki zaidi ya 10,000 kutoka kampuni zaidi ya 2,050 katika nchi na maeneo 80 duniani kote, kwa mujibu wa S&P Global.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha