Chapa za midoli za China zavutia wimbi kubwa la ufuatiliaji kwenye Maonyesho ya Midoli jijini New York

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 05, 2025
Chapa za midoli za China zavutia wimbi kubwa la ufuatiliaji kwenye Maonyesho ya Midoli jijini New York
Watembeleaji wakitembelea Banda la China kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Midoli ya Amerika Kaskazini Mwaka 2025 mjini New York, Marekani, Machi 2, 2025. (Xinhua/Liu Yanan)

NEW YORK - Wauzaji zaidi ya 80 wa midoli kutoka China wamepeleka bidhaa zaidi ya 1,000 kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Midoli ya Amerika Kaskazini Mwaka 2025 katika Jiji la New York, Marekani, zikivutia wimbi kubwa la ufuatiliaji kutoka kwa wanunuzi wa kimataifa.

Maonyesho hayo ya siku nne ambayo yamemalizika jana Jumanne yalivutia watengenezaji, wauzaji reja reja, wawakilishi wa mauzo na wengine kutoka tasnia ya midoli kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Banda la China lilivutia watu wengi kwa miundo ya kipekee ya bidhaa, miongoni mwao imechochewa na utamaduni wa jadi wa China.

Chapa ya midoli ya China ya Bazuuyu pamoja na Kampuni ya Kutengeneza Midoli ya Dongguan Yuankang zimegeuza mambo mbalimbali ya chakula cha hotpot kuwa miundo ya midoli ya kuchezea.

Watembeleaji wa banda hilo walishiriki katika mchezo wa kuiga mchakato wa kuandaa hotpot ya Kichina. Ubunifu wa chapa hiyo umepata "Tuzo ya Nguvu Kubwa ya Kuchezea" kutoka kwenye maonyesho hayo.

"Ninajivunia sana kuleta utamaduni wa chakula wa China nchini Marekani kwa wateja wengi zaidi wa kimataifa," amesema mwanzilishi wa Bazuuyu Zhang Guoping, ambaye anatoka Mkoa wa Sichuan wa China, ambao ni chimbuko la hotpot ya pilipili ya China.

52Toys, chapa ya midoli yenye makao yake Beijing, imepeleka midoli mingi yenye ubunifu wa utamaduni wa China inayopendwa na watu, kama vile masanduku ya mshangao yenye midoli ya panda wanaopiga makasia ya mashua ya dragoni katika Sikukuu ya Mashua za Dragoni, na uchoraji wa wino wa kijadi wa Kichina.

Sera za ushuru zilizoletwa na utawala wa Trump zimeleta changamoto mpya kwa watengenezaji midoli. Huku wakibuni miundo ya bidhaa, watengenezaji midoli wa China pia wanafikiria upya mikakati ya bei na uzalishaji ili kukabiliana na ushuru huo mpya kutoka Marekani.

Deng Xiaocheng, mwanzilishi wa Kampuni ya Biashara ya Jiangsu Comco amesema kuwa soko la Marekani ni moja ya masoko yake muhimu zaidi, likichangia asilimia 40 ya jumla ya biashara ya midoli ya kampuni hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu asilimia 80 ya midoli inayouzwa nchini Marekani inatengenezwa nchini China. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha