Kenya yatoa wito wa ufadhili bunifu ili kulinda wanyamapori

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 04, 2025
Kenya yatoa wito wa ufadhili bunifu ili kulinda wanyamapori
Rebecca Miano, waziri wa Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Kenya, akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani katika Kaunti ya Baringo, magharibi mwa Kenya, Machi 3, 2025. (Xinhua/Han Xu)

BARINGO, Kenya - Kenya imeadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani jana Jumatatu, huku maafisa wake waandamizi wakitoa wito wa matumizi ya mifumo bunifu ya ufadhili ili kulinda spishi za kipekee za viumbepori katikati ya ongezeko la matishio kutoka katika kupotea makazi, ujangili na mabadiliko ya tabianchi.

Rebecca Miano, waziri wa Wizara ya Utalii na Wanyamapori ya Kenya, amesema kuwa ufadhili wa jadi wa umma pekee hautoshi kukabiliana na matishio yanayoongezeka kwa urithi wa wanyamapori wa nchi hiyo.

"Mifumo bunifu ya ufadhili kama vile mikopo ya wanyamapori, dhamana za uhifadhi na ubadilishaji wa madeni kwa mazingira ya asili zinaweza kuziba pengo la ufadhili na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi," Miano amesema katika hafla ya Siku ya Wanyamapori Duniani iliyofanyika Kaunti ya Baringo, eneo lililoteuliwa na UNESCO la Ramsar magharibi mwa Kenya.

Amesema kuwa Kenya inalenga kuhamasisha uhifadhi kwa kubuni mifumokazi ambayo hutoa malipo kwa jamii au wamiliki wa ardhi ambao hulinda makazi ya wanyamapori kupitia huduma kama vile uhifadhi kaboni na uchujaji maji, zikiunga mkono uhifadhi wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka.

Erustus Kanga, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Wanyamapori la Kenya, amesema kuwa ufadhili bunifu wa uhifadhi utachangia katika malengo ya maendeleo ya taifa, kupunguza umaskini, usawa wa kijinsia na kuhimili tabianchi.

Kanga ameongeza kuwa miundo ya utalii endelevu, kama vile utalii wa mazingira, inaweza kuzalisha mapato kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, huku mapato hayo yakielekezwa katika juhudi za uhifadhi, maendeleo ya jamii na hatua za kupambana dhidi ya ujangili.

Kwenye maadhimisho hayo ya Siku ya Wanyamapori Duniani, maafisa wa Kenya wamezindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Spishi Moja kwa Ndege Korongo wa Kijivu. Kwa mujibu wa Miano, spishi hizo za ndege zilizo katika hatari ya kutoweka zimekuwa zikikabiliwa na upungufu wa haraka wa idadi yao wa hadi asilimia 80 katika kipindi cha miaka 50 iliyopita katika makazi yao barani Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha