

Lugha Nyingine
Mkutano wa Usalama wa Munich wafungwa huku kukiwa na uhusiano wenye wasiwasi kati ya nchi za Atlantiki
![]() |
Picha hii ikionyesha nembo iliyofunikwa na theluji ya Mkutano wa Usalama wa Munich mjini Munich, Ujerumani, Februari 16, 2025. (Xinhua/ Zhang Fan) |
MUNICH, Ujerumani - Mkutano wa 61 wa Usalama wa Munich (MSC) umefungwa mjini Munich, Ujerumani Jumapili huku kukiwa na uhusiano wenye wasiwasi kati ya nchi za Atlantiki. “Tunapaswa kuwa na wasiwasi kwamba msingi wetu wa maadili si wa pamoja tena," Christoph Heusgen, mwenyekiti wa MSC, amesema siku hiyo ya Jumapili, akitolea mfano tofauti zinazoongezeka kati ya Ulaya na Marekani, wakati akifunga mkutano huo wa siku tatu.
Kufuatia hotuba yenye utata ya Makamu Rais wa Marekani J.D. Vance katika MSC, Heusgen ameelezea shukrani zake kwamba wanasiasa wa Ulaya "wamezungumza na kusisitiza tena maadili na kanuni wanazozitetea."
Katika mkutano huo, washiriki, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali wapatao 60 na mawaziri 150, walijadili changamoto kuu za usalama wa kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi, usalama wa Ulaya na migogoro ya kikanda.
Hata hivyo, migawanyiko imeendelea katika masuala kama vile mgogoro wa Ukraine na ulinzi wa Ulaya, huku kukiwa na mazingira magumu yanayoongezeka ya siasa za kijiografia.
“Kilichofanya MSC ya mwaka huu kuwa ya kipekee ni maoni ya Vance kuhusu demokrasia na uhuru wa kujieleza barani Ulaya, ambayo yamezua upinzani mkubwa na kufichua wazi mgawanyiko kati ya Marekani na washirika wake wa nchi za Atlantiki,” Xiao Qian, naibu mkuu wa Kituo cha Usalama na Mkakati wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Tsinghua, cha China, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Heusgen amesisitiza hitaji la dharura kwa kujenga desturi na kanuni za pamoja katika dunia yenye ncha nyingi. "Utaratibu huu ni rahisi kuvurugika na kuharibika, lakini ni ngumu kuujenga upya," amebainisha.
Akiangazia kuongezeka kwa umuhimu wa Nchi za Kusini, Heusgen amehitimisha kuwa asilimia zaidi ya 30 ya wazungumzaji katika mkutano wa mwaka huu walikuwa kutoka Afrika, Asia, Amerika ya Kusini, ikihakikisha sauti zao zinasikika katika majadiliano juu ya utaratibu unaobadilika wa dunia yenye ncha nyingi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma