Rais Xi Jinping azungumza na Rais Putin, akitoa wito kwa China na Russia kulinda usawa na haki duniani (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 22, 2025
Rais Xi Jinping azungumza na Rais Putin, akitoa wito kwa China na Russia kulinda usawa na haki duniani
Rais wa China Xi Jinping akizungumza na Rais wa Russia Vladimir Putin kwa njia ya video kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing China, Januari 21, 2025. (Xinhua/Rao Aimin)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping jana Jumanne kwenye mkutano kwa njia ya video amesema anapenda kufanya ushirikiano na Rais wa Russia Vladimir Putin katika kuendelea kuongoza uhusiano wa pande mbili kuelekea ngazi mpya katika Mwaka Mpya.

Rais Xi amesisitiza kuendana na hali ya kutokuwa na uhakika ya mazingira ya nje kwa kutegemea utulivu na uhimilivu wa uhusiano kati ya China na Russia, kuhimiza kwa pamoja maendeleo na ustawishaji wa nchi hizo mbili, na kulinda usawa na haki duniani.

Wakuu hao wawili wa nchi wamepeana salamu za sikukuu ya Mwaka Mpya ujao wa Jadi wa China.

Rais Xi amekumbuka mikutano mitatu aliyofanya na Rais Putin mwaka jana, ambapo wamepata maoni mengi muhimu ya pamoja. Pia ameelezea shughuli mbalimbali zilizofanyika ikiwa ni sehemu ya Miaka ya Utamaduni ya China na Russia, vilevile kuendeleza kwa utulivu ushirikiano wa kivitendo na kukuza biashara ya pande mbili.

"Uratibu wa karibu kati ya nchi hizo mbili kwenye majukwaa ya pande nyingi kama vile Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) na BRICS umetoa nishati chanya zaidi kwa mageuzi na maendeleo ya mfumo wa usimamizi wa Dunia," Rais Xi amesema.

Ametoa wito kwa pande hizo mbili kuendelea kuzidisha uratibu wa kimkakati, kuimarisha kuungana mkono, na kulinda maslahi halali ya nchi hizo mbili."China na Russia zinapaswa kuimarisha na kupanua uhusiano wa pande mbili na kusukuma mbele maendeleo ya kina ya ushirikiano wenye matokeo halisi," Rais Xi ameongeza.

Amesema kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 80 tangu ushindi wa Vita vya Watu wa China vya kupambana na Uvamizi wa Japan, Vita Vikuu vya Kulinda Nchi vya Umoja wa Kisovieti na Vita vya Dunia vya Kupambana na Ufashisti, pamoja na maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

“China na Russia zinapaswa kutumia fursa hii kulinda kwa pamoja mfumo wa kimataifa ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa na kulinda matokeo ya ushindi katika Vita vya Pili vya Dunia, kuhimiza nchi zote kutekeleza kwa makini nia na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa, kushikilia kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa zinazotambulika duniani, na kutekeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi,” Rais Xi amesisitiza.

Kwa upande wake Rais Putin amesema Russia na China siku zote zimekuwa zikipeana imani na kuungana mkono, na kutendeana kwa usawa, na ushirikiano kati ya pande hizo mbili ni kwa maslahi ya watu wa nchi hizo mbili na haujaathiriwa na mabadiliko ya hali ya kimataifa.

Ameeleza kuridhishwa na mwelekeo mzuri unaoendelea katika biashara ya pande mbili na ushirikiano wa nishati, ongezeko tulivu la idadi ya watalii kutembeleana katika nchi hizo mbili, na mawasiliano ya karibu kati ya pande hizo mbili kwenye ushirikiano wa pande nyingi.

Wakuu hao wawili wa nchi pia wamebadilishana mawazo kwa kina kuhusu masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa kwa pamoja, na kukubaliana kudumisha mawasiliano ya kimkakati katika mwaka mpya.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha