

Lugha Nyingine
Tamasha la Teknolojia la Afrika, Africa Tech Festival 2024 laanza mjini Cape Town, Afrika Kusini (2)
![]() |
Watu wakihudhuria Tamasha la Teknolojia la Afrika, Africa Tech Testival 2024 mjini Cape Town, Afrika Kusini, Novemba 12, 2024. (Picha na Fred Barker/Xinhua) |
CAPE TOWN - Tamasha la Teknolojia la Afrika, Africa Tech Festival 2024 limeanza Jumanne mjini Cape Town, mji mkuu wa kibunge wa Afrika Kusini, likikutanisha pamoja viongozi wa kimataifa wa teknolojia na mawasiliano ya simu, wajasiriamali, na watunga sera.
Tamasha hilo, mojawapo ya matukio makubwa na yenye ushawishi mkubwa zaidi katika sekta ya mawasiliano ya simu na teknolojia barani Afrika, linalenga kuleta mageuzi ya kidijitali na uvumbuzi katika bara zima.
Likifanyika sasa kwa awamu yake ya 27, tamasha hilo la mwaka huu, lililoanza Novemba 12 na litaendelea hadi kesho Novemba 14 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Cape Town, linashirikisha shughuli nne muhimu: AfricaCom, AfricaTech, AfricaIgnite, na Mkutano wa AI wa Cape Town. Linatarajiwa kuvutia watu zaidi ya 15,000, waonyeshaji bidhaa zaidi ya 300, na wazungumzaji 450 kutoka bara hilo na sehemu nyingine.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia za Kidijitali wa Afrika Kusini Solly Malatsi akihutubia ufunguzi wa tamasha hilo siku ya Jumanne ametoa wito wa juhudi za pamoja ili kuendeleza mustakabali wa kidijitali wa Afrika.
"Leo, tunasimama kwenye ukingo wa fursa za kimageuzi. Zama ya kidijitali imefungua milango ya ukuaji na ujumuishaji katika bara zima, ikitengeneza njia mpya za maendeleo ya kiuchumi na kijamii," Malatsi amesema.
Waziri huyo amesema kuwa Afrika Kusini inajitahidi kujenga uchumi wa kidijitali. "Hata hivyo, hatuwezi kufikia dira hii kupitia juhudi za serikali pekee. Inahitaji ushirikiano katika sekta nzima. Ninaalika washirika wetu wote kuleta utaalamu, mawazo, na suluhu zao ili kuendeleza mustakabali wa kidijitali wa Afrika."
Akirejelea utafiti mbalimbali, Malatsi amesema kuwa kufikia asilimia 100 ya kupenya kwa intaneti katika nchi za Afrika za Kusini mwa Sahara kunaweza kuongeza ukuaji wa uchumi wa kanda hiyo kwa nyongeza ya asilimia 1.5 kila mwaka, kutengeneza mamilioni ya fursa za ajira na kuendesha ujumuishaji wa kiuchumi. Muunganisho wa intaneti kwa wote barani Afrika unaweza kuinua watu zaidi ya milioni 44 kutoka kwenye umaskini uliokithiri, amesema.
"Kwa pamoja, tutajenga Afrika ambapo teknolojia itawawezesha watu wake wote, waliounganishwa na kunufaisha ukuaji na mafanikio kwa pande zote," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma