

Lugha Nyingine
China yarusha satelaiti mpya kwenye anga ya juu ili kuboresha huduma za BDS-3
XICHANG - China imerusha kwa mafanikio satelaiti mbili mpya za mfumo wa Satelaiti BeiDou-3 (BDS-3) kwenye anga ya juu kutoka Kituo cha Urushaji Satelaiti kwenye Anga ya juu cha Xichang kilichoko Mkoa wa Sichuan, Kusini Magharibi mwa China, ambapo satelaiti hizo mbili, satelaiti ya 57 na 58 za mfumo wa BeiDou, zimerushwa majira ya saa 5:26 asubuhi (kwa saa za Beijing) kwa kutumia roketi ya Long March-3B na chombo cha msukumo wa kwenda juu cha Yuanzheng-1 (Expedition-1) kilichowekwa kwenye roketi ya kubeba.
Hizi ni satelaiti za kwanza za obiti ya Dunia ya kati (MEO) kurushwa tangu mfumo wa BDS-3 ulipoidhinishwa rasmi kutoa huduma duniani kote. Baada ya kuingia kwenye obiti yao na kukamilisha majaribio ya obiti, zitaunganishwa kwenye mfumo wa BeiDou.
Ikilinganishwa na satelaiti za awali za MEO za mfumo wa BeiDou, satelaiti hizi mpya zilizorushwa zimeboreshwa kwa utendaji na ufanisi wake katika uwezo wa mawasiliano wa ujumbe mfupi wa kimataifa, teknolojia ya saa ya atomiki, na upakiaji mzigo kwa kutumia teknolojia za akili bandia.
Vilevile hali ya kuaminika na uwezo wa huduma wa mfumo wa BeiDou pia utaboreshwa na kupanda ngazi ya juu. Na zitaweka msingi wa uundaji wa satelaiti za BDS za kizazi kijacho.
Urushaji huo ni safari ya 504 ya roketi za mfululizo za Long March.
Satelaiti hizo na chombo chake cha kuzirusha vimeundwa na Taasisi Kuu ya Teknolojia ya Anga ya Juu ya China (CAST) na Taasisi Kuu ya China ya utafiti wa teknolojia za maroketi, ambazo zote ni za Shirika la Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu la China.
Satelaiti hizi mbili zitatekeleza majukumu mengi kwa kupanua kwa ufanisi uwezo wa BeiDou wa mawasiliano ya kimataifa kwa ujumbe mfupi, amesema Xie Jun, Naibu Msanifu Mkuu wa BDS.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma