Rais Xi Jinping asema hakuna nchi inapaswa kuachwa nyuma katika maendeleo ya kisasa ya Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 25, 2023
Rais Xi Jinping asema hakuna nchi inapaswa kuachwa nyuma katika maendeleo ya kisasa ya Dunia
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba yenye kichwa cha "Kushikana mikono Kuelekea Jumuiya ya Maendeleo ya Pamoja" kwenye Mazungumzo ya nchi za BRICS na Afrika na BRICS Plus huko Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 24, 2023. (Xinhua/Li Xueren)

JOHANNESBURG - Rais Xi Jinping wa China ametoa wito wa kufanyika kwa juhudi za pamoja katika kujenga jumuiya ya maendeleo ya pamoja, na kuhakikisha kwamba hakuna nchi inayoachwa nyuma katika mchakato wa maendeleo ya kisasa ya Dunia.

Rais Xi ametoa wito huo siku ya Alhamisi kwenye Mkutano wa Mazungumzo ya nchi za BRICS na Afrika na BRICS Plus uliofanyika hapa pembezoni mwa Mkutano wa 15 wa wakuu wa BRICS.

“Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa bado unaendelea polepole,” Rais Xi amebainisha, huku akisema kwamba hili ni suala la kutia wasiwasi na kufuatilia, na jitihada za maendeleo ya kimataifa zinakabiliwa na changamoto kubwa.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufuatilia maslahi makubwa ya nchi zote, kukabiliana na matatizo ya watu, kurejesha suala la maendeleo kwenye katikati mwa ajenda ya kimataifa, na kufanya jitihada za kuongeza uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea katika utawala wa kimataifa na kusaidia nchi zinazoendelea katika kufikia maendeleo bora zaidi.

"Pia ni muhimu kushikilia ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, kujenga ushirikiano wa maendeleo wa kimataifa, na kuweka mazingira salama na tulivu ya kimataifa kwa maendeleo ya pamoja," Rais Xi ameongeza.

"Nilipendekeza Mpango wa Maendeleo ya Dunia (GDI), haswa kwa madhumuni ya kutoa wito kwa Dunia kuendelea kujikita katika maendeleo na kutoa msukumo kwa utekelezaji wa Ajenda ya 2030," Rais Xi ameeleza.

Huku akisisitiza kuwa China imeweka maendeleo kuwa kipaumbele na kutenga rasilimali zaidi, Rais Xi amesema nchi hiyo imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kusini na Kusini wenye ufadhili wa jumla ya dola za kimarekani bilioni 4.

"China ni rafiki anayetegemeka wa Afrika," Rais Xi amesema.

Katika kipindi kijacho, China itafanya ushirikiano zaidi na nchi za Afrika ili kuisaidia Afrika katika kuongeza uwezo wake wa maendeleo ya kujitegemea, Rais Xi amesema, huku akiongeza kuwa, taasisi za kifedha za China zitaunda mfuko maalum wa dola bilioni 10 kwa ajili ya utekelezaji wa GDI.

Mkutano huo umeandaliwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, na pia kuhudhuriwa na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi. Rais wa Russia Vladimir Putin alishiriki mtandaoni.

Zaidi ya viongozi 60 na wawakilishi wa nchi za Afrika na nchi nyingine zenye masoko yanayoibukia na zinazoendelea, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Benki Mpya ya Maendeleo Dilma Rousseff, na viongozi wa mashirika mengine ya kimataifa na kikanda, pia walihudhuria.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha