Kampuni kubwa ya mafuta ya China yachangia kuwaandaa vijana wenye vipaji kutumikia sekta ya mafuta inayoanza Uganda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 10, 2023
Kampuni kubwa ya mafuta ya China yachangia kuwaandaa vijana wenye vipaji kutumikia sekta ya mafuta inayoanza Uganda
Picha hii iliyopigwa Januari 24, 2023 ikionyesha eneo la kuchimba mafuta la Kingfisher huko Kikuube, Uganda. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

KIKUUBE – Katika mwambao wa Ziwa Albert katikati mwa Afrika, ambao unatumiwa kwa pamoja na Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kampuni kubwa za kimataifa za mafuta za China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) na French TotalEnergies, ambazo Februari mwaka jana zilitangaza Uamuzi wa Mwisho wa Uwekezaji (FID) kuanza uzalishaji wa kibiashara wa mafuta nchini Uganda zinashughulika na maandalizi ya kuanza uzalishaji wa mafuta wa kwanza kabisa nchini Uganda.

Emmanuella Kaducu, ni mmoja wa wanafunzi wa chuo kikuu cha mafuta na gesi nchini Uganda ambaye ameshinda shindano la kitaifa kuhusu sekta ya mafuta inayoanza kwa sasa nchini humo. Mojawapo ya zawadi za shindano hilo ni safari ya kutembelea visima vya mafuta katika eneo la mafuta la Kingfisher katika Wilaya ya Kikuube, Mkoa wa Magharibi wa Uganda, na eneo la mafuta la Tilenga katika eneo jirani la Buliisa.

Huko Kingfisher, Kaducu na washindi wengine walikutana na wataalam wenyeji watakaokuwa wenzao wa baadaye wa mafuta ambao tayari wanafanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi.

Kaducu ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi majuzi kwamba alipata msukumo mkubwa kutoka kwa wataalamu vijana, na hii inaimarisha azma yake ya kumaliza kozi yake ya sayansi ya petroli na uzalishaji wake katika chuo kikuu.

Linette Naiga, mhandisi kijana wa kuchimba mafuta katika mashine kwenye moja ya visima vya mafuta huko Kingfisher ambaye alizungumza na Kaducu na marafiki zake, amesema wataalamu vijana wanaongezeka katika kuchukua nyadhifa kwenye sekta changa ya mafuta nchini humo.

"Kufanya kazi na Wachina ni jambo la kuridhisha sana, kuna mengi ya kujifunza, kuna uhamishaji wa teknolojia nyingi. Ni changamoto ingawa ina thawabu, inanisukuma kila siku kufikia uwezo wangu," amesema Ambrose Ogwang, mmoja wa wafanyakazi wenzake na Naiga.

Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda imesema, Mradi huo wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 10, unaohusisha uendelezaji wa visima vya mafuta na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi litakalosafirisha mafuta hayo kutoka magharibi mwa Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445, linalokadiriwa kugharimu dola bilioni 3.55 za Kimarekani, litakuwa bomba refu zaidi duniani lenye kusafisha mafuta ya moto. Wizara hiyo imekadiria kuwa, baada ya kukamilika kwa ujenzi, utoaji wa mafuta wa mara ya kwanza utapatikana mwaka 2025 nchini humo. Mradi huo utatoa nafasi za ajira zipatazo 160,000 mbali na ajira za utoaji wa bidhaa na huduma.

Mwaka 2006 Uganda iligundua uwepo wa mafuta yenye ujazo wa mapipa bilioni 6.5, ambapo mapipa bilioni 1.4 yana uwezo wa kuuzwa kibiashara, wizara hiyo imesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha