

Lugha Nyingine
IEA yasema uwekezaji katika ufanisi wa nishati duniani unahitaji kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2030
PARIS - Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) limesema siku ya Jumatano kwamba, uwekezaji wa kila mwaka katika kuboresha ufanisi wa nishati lazima uongezeke mara tatu ifikapo Mwaka 2030 ili Dunia ibaki na uwezo wa kuweka joto duniani chini ya nyuzi joto 1.5.
Ukichochewa na matumizi katika majengo na mauzo ya magari yenye kutumia nishati ya umeme, uwekezaji katika ufanisi wa nishati duniani ulifikia rekodi ya dola za Marekani bilioni 600 Mwaka 2022, IEA imesema katika ripoti yake iliyopewa jina la Ufanisi wa Nishati: Muongo wa Hatua.
IEA imeonya kuwa, Mwaka 2023 kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 624, lakini kiwango cha ukuaji kitakuwa chini kuliko Mwaka 2022 kwani gharama ya juu ya mtaji inalemea sana miradi mipya inayoweza kutarajiwa.
Katika ripoti yake hiyo iliyochapishwa kwenye Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Ufanisi wa Nishati wa IEA, shirika hilo limesema kwamba kuongeza maradufu kwa maendeleo ya ufanisi wa nishati hadi asilimia 4 kila mwaka ifikapo Mwaka 2030 kutahitaji uwekezaji katika sekta hiyo kupanda kutoka dola bilioni 600 hadi zaidi ya dola trilioni 1.8. za Kimarekani kufikia Mwaka 2030.
Shirika hilo limesisitiza kuwa lengo la asilimia 4 ifikapo Mwaka 2030 litatoa punguzo muhimu katika utoaji wa hewa chafu na wakati huo huo kuongeza nafasi za kazi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, shughuli za ufanisi wa nishati zinaweza kutoa nafasi za ajira milioni 12 duniani kote ifikapo Mwaka 2030.
"Muhimu zaidi, mahitaji zaidi ya nishati fanisi na ya chini yanasaidia maendeleo ya haraka kuelekea upatikanaji wa nishati ya kisasa na ya bei nafuu katika nchi zinazoibukia na zinazoendelea," imeeleza.
Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa IEA kuhusu Ufanisi wa Nishati unafanyika mjini Paris Juni 7 hadi Juni 8. Lengo ni kuharakisha maendeleo ya ufanisi wa nishati.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma