Timu ya madaktari wa China yatoa mafunzo kwa madaktari wa Zambia kuondoa uvimbe kwenye ubongo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 28, 2023
Timu ya madaktari wa China yatoa mafunzo kwa madaktari wa Zambia kuondoa uvimbe kwenye ubongo
Chen Zhenbo (wa kwanza, kulia), mtaalam wa afya wa Timu ya Madaktari wa China, akieleza uzoefu wake katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Lusaka cha Zambia, Februari 24, 2023. Madaktari wa Zambia wamefanikiwa kufanya upasuaji mara nne ili kuondoa uvimbe kwenye ubongo baada ya kupewa mafunzo yaliyofanywa na Timu ya 23 ya Madaktari wa China, daktari mwandamizi wa upasuaji wa neva katika hospitali kubwa zaidi nchini humo alisema Ijumaa. (Xinhua/Peng Lijun)

LUSAKA - Kachinga Sichizya, daktari mwandamizi wa upasuaji wa neva katika hospitali kubwa zaidi nchini Zambia Ijumaa alisema kwamba madaktari wa nchi hiyo wamefanikiwa kufanya upasuaji mara nne ili kuondoa uvimbe kwenye ubongo baada ya kupewa mafunzo yaliyofanywa na Timu ya 23 ya Madaktari wa China.

Sichizya, ambaye ni mkuu wa upasuaji katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Lusaka, amesema madaktari vijana wa eneo hilo wamefanikiwa kufanya upasuaji wa kupitia tundu za pua (transnasal) ili kuondoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia endoscope kwa wagonjwa chini ya usimamizi wa Chen Zhenbo, mtaalam wa tiba wa timu ya madaktari wa China.

"Hii imekuwa wiki muhimu katika historia ya upasuaji wa mishipa ya fahamu nchini Zambia kwa sababu tumeweza kufanya oparesheni nne kupitia njia ya pituitari. Ni operesheni ngumu sana," Sichizya amesema pembezoni mwa mkutano wa kimataifa wa upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo ulioandaliwa kwa lengo la kubadilishana mawazo na uzoefu kati ya madaktari wa China na wenzao wa Zambia.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na baadhi ya madaktari wanafunzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zimbabwe na Botswana.

Sichizya ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba upasuaji huo uliandaliwa kufuatia kukamilika kwa mafunzo ya miezi kadhaa ambapo Daktari Chen aliwafundisha madaktari wa eneo hilo kufanya upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia endoscopic kupitia tundu za pua.

Amesema madaktari hao chini ya uangalizi wa Chen wamekuwa wakijiandaa kwa ajili ya upasuaji huo katika muda wa miezi miwili iliyopita, na kuongeza kuwa kufanikiwa kwa upasuaji huo ni kielelezo kuwa madaktari wa eneo hilo sasa wataweza kufanya upasuaji huo hata pale madaktari wa China watakapoondoka mwezi ujao.

Yan Hongxian, kiongozi wa Timu ya Madaktari wa China, amesema ni nia na shauku kubwa kwa timu za madaktari kutoka China kutoa ujuzi wa hali ya juu kwa wenzao wenyeji. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha