Wasichana na Wanawake wa Tanzania wakumbatia sayansi na teknolojia katika kuendesha uchumi wa kidijitali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 13, 2023
Wasichana na Wanawake wa Tanzania wakumbatia sayansi na teknolojia katika kuendesha uchumi wa kidijitali
Wanawake wakichukua masomo ya kutengeneza programu za kompyuta jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 8, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

DAR ES SALAAM - Jacqueline Msambila, msichana wa Tanzania mwenye umri wa miaka 24, aliamka mapema asubuhi na kuazimia kuungana na wasichana na wanawake wengine duniani kote kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi.

Msambila, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayesoma shahada ya uzamili ya sanaa katika maadili ya utawala bora na utumishi wa umma, aliadhimisha siku hiyo kwa kuwataka wasichana na wanawake wenzake nchini Tanzania kuchangamkia sayansi na teknolojia katika kusaidia lengo la nchi hiyo ya Afrika Mashariki la uchumi wa kidijitali.

Kwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi ni tukio la kila mwaka ambalo huadhimishwa Februari 11 na ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuwahimiza wanawake waweze kupata nafasi na kushiriki kwa kutosha katika sekta za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), Msambila anaamini kuwa pengo kubwa kati ya wanaume na wanawake, linapokuja suala la maarifa juu ya sayansi na teknolojia, linaweza kupunguzwa ikiwa wanawake wataweka juhudi na nguvu zaidi katika kupata taaluma hizo mbili.

Na uamuzi huo ndiyo ulimsukuma mwanafunzi huyo kijana wa chuo kikuu kujiunga na masomo ya kuandika msimbo yanayotolewa bila malipo na Taasisi ya Launchpad Tanzania, asasi ya kiraia inayojikita kwenye programu za maendeleo ya wanawake na vijana, yenye makao yake makuu katika Jiji la Dar es Salaam.

Msambila ni miongoni mwa wasichana na wanawake 36 wenye umri kati ya miaka 18 na 30 wanaohudhuria masomo ya usimbaji, kufanya biashara kidijitali na ubunifu wa michoro, miongoni mwa mengine, kwenye ofisi kuu za Launchpad Tanzania zilizoko katika Kitongoji cha Sinza.

"Tunataka kuibua hadithi ya wasichana hawa wanaopata mafunzo haya na namna yatakavyoongeza ushiriki wao na kuziba pengo la mgawanyiko wa jinsia kidijitali kwa kuwa na wanawake Watanzania wenye ujuzi zaidi katika uchumi wa kidijitali," Loy Harold Jaffu, meneja wa laini ya usaidizi wa Launchpad Tanzania, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake ni siku inayoadhimisha mafanikio ya wanawake kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Siku hiyo pia inaashiria mwito wa kuchukua hatua ili kuharakisha usawa wa wanawake.

"Kwa kuwa wanawake ni nusu ya idadi ya Watanzania wote, wana ushawishi mkubwa wa kuwa viongozi wanaoongoza katika kusukuma uchumi wa kidijitali," amesema Msambila kwa kujivunia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha