

Lugha Nyingine
Wanaanga wa China wazungumza wakiwa anga ya juu na vijana wa nchi mbalimbali za Afrika
CAIRO - Wanaanga watatu wa China Jumanne wiki hii walizungumza wakiwa anga ya juu na vijana kutoka nchi nane za Afrika kwa njia ya video, wakibadilishana uzoefu wao katika misheni ya Chombo cha anga ya juu cha China cha Shenzhou-14.
Wanaanga hao Chen Dong, Liu Yang na Cai Xuzhe, ambao wako kwenye safari ya obiti ya miezi sita, waliwaonesha vijana wa nchi za Afrika maisha yao na kazi ya kisayansi katika kituo cha anga ya juu.
Ukumbi mkuu wa shughuli hiyo iliyopewa jina la "Ongea na Wanaanga," ulikuwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia huku wanafunzi kutoka Algeria, Misri, Ethiopia, Namibia, Nigeria, Senegal, Somalia na Afrika Kusini wakishiriki katika mhadhara huo kwenye kumbi ndogo.
Emily Nangacovie, mwanafunzi wa sayansi kutoka Namibia, alipata fursa ya kuuliza maswali kuhusu utafiti gani wamefanya katika misheni yao.
Akijibu swali hilo, Mwanaanga Cai amesema kwamba wamekuwa "wakilenga kusoma athari za mfiduo wa muda mrefu wa mvuto sifuri kwa afya ya wanaanga na hatua zinazoendana za ulinzi wa afya, wakiangalia tabia na uwezo wa wanaanga na kubobea katika matumizi ya dawa za mitishamba angani."
"Na (sisi) pia tunafanya majaribio juu ya sayansi ya mvuto unaobadilika, sayansi ya maisha na ikolojia, sayansi ya teknolojia ya kibayoteknolojia, fizikia ya maji na sayansi ya mwako," Cai ameongeza.
"Miradi hii ya majaribio ya utafiti itatoa msaada kwa wanaanga kuishi maisha yenye afya na kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu katika kituo cha anga ya juu na kuweka msingi wa uchunguzi wa siku zijazo katika anga ya juu," ameelezea.
Chen, mwanaanga mwingine wa China, amesema "watafanya shughuli za ziada, matengenezo ya vifaa vya obiti, majaribio ya matumizi ya anga ya juu, majaribio ya matibabu ya anga ya juu, na mihadhara ya kituo, kati ya kazi zingine."
Naye Kaimu Balozi wa Ubalozi wa China nchini Namibia, Yang Jun, amesema China itasaidia kutoa mafunzo kwa mafundi wa Namibia kuhusu teknolojia ya anga ya juu na itafanya utafiti wa anga ya juu kwa pamoja na Namibia.
Mwaka jana wanaanga watatu wa China kwenye chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-12 walibeba bendera ya taifa ya Namibia wakiwa angani, wakati wanaanga wawili Cheng na Liu, walitembelea Namibia Mwaka 2019.
"Tunaweza kuona jinsi ushirikiano wa anga ya juu kati ya China na Namibia ulivyo na matunda," Yang amesema, huku akiongeza kuwa kazi ya kuendeleza teknolojia ya anga ya juu ni jukumu la vijana duniani.
Katika kumbi hizo mbalimbali za shughuli hiyo, wanafunzi wengi wa Afrika wameonesha shauku kubwa ya kufahamau ujuzi na shughuli za wanaanga wa China. Lakini pia walionesha shauku ya kujifunza zaidi kuhusu teknolojia ya anga ya juu na kuelezea ndoto zao za kuwa sehemu ya vijana watakaobeba jukumu la kushiriki kwenye ujenzi wa anga ya juu.
Mabalozi wa China katika nchi husika na viongozi mbalimbali wa Afrika walishiriki kwenye shughuli hiyo ambayo ni ya kwanza na ya aina yake kuwahi kufanyika barani Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma