

Lugha Nyingine
Mwanaanga wa kike wa China atuma salamu za Siku ya Kimataifa ya Wanawake kutoka anga ya juu (3)
![]() |
(Picha kutoka Xinhua) |
GENEVA - Wang Yaping, mwanaanga wa pili wa kike wa China ambaye sasa yuko katika safari ya miezi sita kwenye Kituo cha Anga cha nchi hiyo, hivi karibuni alipiga video kwa ajili ya ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) huko Geneva, Uswisi, akitoa salamu zake kwa wanawake duniani kote katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Tarehe 8 Machi.
"Natumai wasichana wote wenye ndoto za kwenda anga ya juu mnalinda maono yenu ya kwenda kwenye bahari ya nyota. Siku moja, kabla ya kujua, unapotazama juu, utaona kwamba ndoto yako tayari imetimia," Wang amesema.
Amesema kuwa anga ya juu haijawahi kubadilisha mazingira yake au kushusha vigezo kwa sababu ya kuwasili kwa wanawake, na kwamba data nyingi za safari za anga ya juu zinaonyesha kuwa hakuna tofauti kubwa za kijinsia katika uwezo kubadilika na kufanya kazi katika anga ya juu.
Wanawake "wote wanaweza kukamilisha mafunzo na tathmini sawa na wanaanga wa kiume kwa kiwango cha juu. Na sifa nyingi za kimwili na kisaikolojia za wanawake zinaweza kuwa na manufaa katika anga ya juu, na kusaidiana na wanaanga wa kiume," amesema.
"Mabibi, pamoja na kwamba uraia, makabila na kazi zetu ni tofauti, lakini wanawake duniani kote wanaifanya Dunia kuwa hai zaidi na yenye usawa na ukarimu zaidi kwa jitihada zao wenyewe," amesema.
"Ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru kila mwanamke kwa kujitolea kwao, pia ninatamani kila mwanamke angechagua nyota bora zaidi kwa maisha na kazi tunazopenda katika anga yetu ya nyota."
Wang na wanaanga wengine wawili waliingia kwenye anga ya juu wakitumia chombo cha Shenzhou-13 na kuingia kwenye kituo cha anga za juu Oktoba 16, 2021, kuanza safari ya anga ya miezi sita.
Watatu hao wamekuwa kwenye obiti kwa zaidi ya siku 130, huku Wang akiweka rekodi ya kukaa siku nyingi zaidi kwenye anga ya juu kwa mwanaanga wa China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma