China kushirikiana na Afrika kukuza matumizi ya Mfumo wa Setilaiti wa Beidou (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 10, 2021
China kushirikiana na Afrika kukuza matumizi ya Mfumo wa Setilaiti wa Beidou

Katika kongamano la kwanza la ushirikiano wa mfumo wa setilaiti wa Beidou kati ya China na Afrika lililofanyika mjini Beijing, China mwishoni mwa wiki iliyopita, washiriki kutoka China na Afrika wamekubaliana kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wao katika kukuza na kutumia Mfumo wa Satelaiti wa kuongoza mawasiliano wa Beidou.

Maafisa, viongozi wa sekta na watafiti kutoka China, nchi za Afrika na Umoja wa Afrika walitoa mawazo yao kwenye Kongamano hilo na kukubaliana kutumia fursa ya mfumo wa Beidou ili kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.

He Yubin, Mwenyekiti wa Kamati ya mfumo wa Satellite wa kuongoza mawasiliano ya China, amesema kwamba kamati yake iko tayari kubadilishana uzoefu na utaalamu wake katika mfumo wa Beidou na Afrika na kufanya kazi na nchi za Afrika kubuni mpango wa matumizi ya mfumo wa Beidou barani Afrika kwa ajili ya maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

"China itashirikiana na Afrika kukuza huduma za Beidou katika Bara la Afrika ili kuendeleza viwanda na biashara za ndani na kusaidia kutoa fursa nyingi za ajira na kupunguza umaskini" amesema.

Xu Hongliang, Katibu Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya Anga ya Juu ya China, amesema kuwa idara yake imejitolea kuchangia mafanikio ya maendeleo ya anga ya juu ya China na Afrika ili kuhimiza maendeleo ya sayansi na teknolojia ya bara hilo. Pia imedhamiria kuboresha mawasiliano na mafunzo ya wataalamu wa sekta ya anga ya juu ili kuwezesha juhudi za nchi za Afrika kukuza uwezo wao wa anga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Sayansi na Teknolojia wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahama Ouedraogo amesema, Beidou itakuwa chombo kikubwa katika maendeleo ya Afrika na anatarajia ushirikiano wa karibu na China katika kuwapa fursa watumiaji wengi wa mfumo wa Beidou barani humo kuongeza kasi katika uchumi wa ndani.

Beidou ni mfumo mkubwa zaidi wa China ulioko anga ya juu na mojawapo ya mifumo minne ya kuongoza mawasiliano ya kimataifa sambamba na ile ya GPS ya Marekani, GLONASS ya Urusi na Galileo ya Umoja wa Ulaya.

Tangu Mwaka 2000, jumla ya satelaiti 59 za Beidou, zikiwemo nne za kwanza za majaribio, zimerushwa kutoka Xichang kwenye roketi 44 za Long March 3, huku baadhi yake zikiwa zimefikia mwisho wa kufanya kazi.

Beidou ilianza kutoa huduma za sehemu, uongozi, muda na ujumbe kwa watumiaji wa kiraia nchini China na maeneo mengine ya eneo la Asia-Pasifiki Mwezi Desemba, Mwaka 2012. Mwishoni mwa Mwaka 2018, ilianza kutoa huduma za kimsingi kote duniani.

Katika kongamano hilo baina ya China na Afrika, jumla ya wawakilishi kutoka karibu nchi 50 za Afrika wakiwemo mawaziri wanane wa serikali na mabalozi wanane nchini China wameshiriki. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha