Lugha Nyingine
Afrika Kusini yatafuta masoko mapya ya mauzo ya nje huku uwezekano wa kupoteza manufaa ya AGOA ya Marekani ukikaribia

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, akijibu maswali ya wabunge katika Baraza la Kitaifa la Majimbo (NCOP), au baraza la juu la bunge, mjini Cape Town, Afrika Kusini, tarehe 24 Novemba 2026. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa nchi hiyo inaongeza juhudi za kutafuta masoko mbadala ya mauzo ya nje na kulinda ajira kutokana na uwezekano wa kupoteza fursa ya kuingiza bidhaa katika soko la Marekani kwa masharti ya upendeleo chini ya Sheria ya Ukuaji na Fursa barani Afrika (AGOA).
Ramaphosa ameyasema hayo Jumanne wiki hii wakati akijibu maswali ya wabunge katika Baraza la Kitaifa la Majimbo bungeni mjini Cape Town, wakati Afrika Kusini inajiandaa kwa uwezekano wa Marekani kuiondoa nchi hiyo hadhi ya kunufaika na mpango huo wa AGOA kuanzia tarehe 1 Januari 2027.
Novemba 2, Marekani iliipa Afrika Kusini notisi ya siku 60 ya kusudio lake la kuondoa hadhi ya kuwa mnufaika wa AGOA; mpango unaozipa nchi zinazostahiki za Afrika ya kusini mwa Sahara fursa ya kuingiza bidhaa katika soko la Marekani kwa masharti ya upendeleo.
Ramaphosa amesema Afrika Kusini imetumia fursa zinazotokana na Mkutano wa 18 wa BRICS, uliofanyika nchini India mwezi Septemba, na shughuli nyingine husika za kibiashara kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa viwanda.
Rais huyo amesema pia Afrika Kusini inatumia fursa ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) ili kupanua aina mbalimbali za bidhaa za kuuzwa nje na kupunguza utegemezi kwa mshirika mmoja wa kibiashara, huku akisisitiza kuwa serikali inafanya kazi ya kuongeza uelewa kuhusu mifumo hiyo ya kibiashara, kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, na kuendeleza minyororo ya thamani ya kikanda.
Ramaphosa amesema kuwa sera ya ushuru-sifuri ya China kwa bidhaa kutoka Afrika inatoa fursa nyingine ya kupanua mauzo ya nje, wakati huohuo Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (SACU) unaendelea na kufikia makubaliano ya hatua za awali za kibiashara na China.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa (kwenye mimbari) akijibu maswali kutoka kwa wabunge katika Baraza la Kitaifa la Majimbo (NCOP), au baraza la juu la bunge, mjini Cape Town, Afrika Kusini, tarehe 24 Novemba 2026. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

Urejeshaji ikolojia waleta uoto wa kijani kwenye kando za Mto Changjiang huko Wuhan, China

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma