Xi asema utafiti wa pamoja wa anga ya juu wa wanaanga wa China na Pakistan waonesha urafiki uliokita mizizi kwa kina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2026

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amesema kuwa utafiti wa pamoja kwenye anga ya juu unaofanywa na wanaanga wa China na Pakistan umeonesha vilivyo urafiki uliokita mizizi kwa kina kati ya nchi hizo mbili.

"Haya ni mafanikio mengine muhimu katika ushirikiano wa pande mbili," amesema Xi wakati akitumiana salamu za pongezi na Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari jana Jumatano kuhusu safari hiyo ya pamoja ya anga ya juu.

Katika salamu zake, Xi amesema amefurahia kupata habari kuhusu mwanaanga wa Pakistan amefanikiwa kufikia kwenye anga ya juu akiwa amepanda chombo cha safari za anga ya juu cha China cha Shenzhou, na kuwa mwanaanga wa kwanza wa kigeni kuingia na kuishi kwenye kituo cha anga ya juu cha China.

Xi ametoa pongezi za furaha kwa serikali ya Pakistan na wananchi wake, pamoja na wanaanga na wataalamu wa safari za anga ya juu wa nchi mbili, akiwa kwa niaba ya serikali ya China na wananchi wake.

Xi ameeleza kuwa China na Pakistan ni washirika wa ushirikiano wa kimkakati wa hali zote, na urafiki kati ya nchi hizo mbili umekuwa imara kama mwamba usiovunjika tangu uhusiano wa kidiplomasia ulipoanzishwa miaka 75 iliyopita.

Akisisitiza kuwa kituo cha anga ya juu cha China ni chombo cha amani, urafiki, na ushirikiano, Xi amesema China inapenda kushirikiana na Pakistan na nchi nyingine katika kuendeleza matumizi ya amani ya anga ya juu, kuzidisha ushirikiano wa kimataifa kwenye nafasi za anga ya juu, na kuboresha usimamizi wa Dunia kwenye anga ya juu, ili kuhakikisha utafiti wa anga ya juu unaleta manufaa mengi zaidi kwa binadamu.

Kwa upande wake, Zardari akiwa kwa niaba ya serikali ya Pakistana na wananchi wake ameeleza shukrani zake za dhati kwa serikali ya China na wananchi wa China walio kama ndugu.

Amesema ushirikiano huo wa kihistoria wa sekta ya anga ya juu kati ya Pakistan na China, na mwanaanga wa kwanza wa Pakistan kuingia kwenye kituo cha anga ya juu cha China, vinajiri wakati nchi hizo mbili zikiadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Zardari amesema, "Ushirikiano wa namna hii unaonesha maendeleo dhahiri ya China katika sayansi na teknolojia ya safari za anga ya juu, na kuonesha China imejikita kwa nia thabiti katika matumizi ya amani ya nafasi kwenye anga ya juu, na pia imeonesha umuhimu wa kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.”

Zardari ameongeza kuwa, ushirikiano huo utaimarisha zaidi urafiki kati ya nchi hizo mbili, na kuendeleza uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa hali zote hadi kwenye kiwango cha juu zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha